Simba yasusa Kariakoo Derby

DAR ES SALAAM: Klabu ya Simba imeamua kutoshiriki mchezo wake wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga SC Jumamosi, Machi 8, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya kudai kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi.
Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Ijumaa, Simba ilieleza kuwa hatua hiyo imetokana na kile ilichokiita ukiukwaji wa kanuni za ligi.
“Simba Sports Club imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana kuelekea mchezo wetu wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga, ambapo Simba ikiwa timu mgeni imenyimwa haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa klabu hiyo, walipofika uwanjani kufanya mazoezi, walizuiwa na meneja wa uwanja aliyedai kuwa hakuwa na maelekezo ya kuwaruhusu. Licha ya kamishna wa mchezo kufika baadaye, Simba inadai kuwa walivamiwa na walinzi binafsi wa Yanga, hali iliyozua sintofahamu kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kuamua kuondoka kwa sababu za kiusalama.
🚨 TAARIFA KWA UMMA. #WenyeNchi #NguvuMoja pic.twitter.com/g2yixaclva
— Simba Sports Club (@SimbaSCTanzania) March 7, 2025
Simba imeitaka mamlaka ya ligi kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na kusisitiza kuwa haitashiriki mechi hiyo.
Kwa mujibu wa kanuni ya 17(45) ya Ligi Kuu Tanzania Bara, timu mgeni inastahili kufanya mazoezi angalau mara moja kwenye uwanja wa mechi kabla ya siku ya mchezo katika muda uliopangwa.
Mpaka sasa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halijatoa tamko rasmi kuhusu suala hilo.



