Tanzania yawa darasa udhibiti mihadarati
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita imepata mafanikio kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema mafanikio waliyopata yameshitua wengi na baadhi ya nchi, ikiwemo Marekani na Uingereza kwani zinakuja kujifunza mbinu wanazotumia.
Lyimo alisema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ni kukamata kilogramu 3,500 (tani 3.5) za dawa za kulevya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
“Haijawahi kutokea wakati wowote kukamata kilo nyingi za dawa za kulevya kama vile, mafanikio haya yanatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kutambua athari zake,” alisema.
Alisema kasi ya kukamata wafanyabishara wa dawa hizo inaendelea na kwa mwaka jana na mwaka juzi walikamatwa 29,187 wakiwemo raia wa kigeni ambao mali zao zimetaifishwa.
“Mpaka sasa kesi zilikuwa 2001 na serikali imeshinda asilimia 80 kwa hiyo unaona tunakwenda vizuri na siku hizi sheria zimebadilisha ukikamatwa hupelekwi kwenu unahukumiwa kwa sheria za hapahapa Tanzania, adhabu yake huwa ni kifungo cha miaka 30 au maisha jela,” alisema Lyimo.
Aliongeza: “Na mpaka sasa tumekamata mitandao saba, mitano ya ndani miwili ya nje… mtandao mmoja inajumuisha watu wengi chini yake kuanzia kinara anayetoa mzigo mpaka wale wanaosambaza, ni watu wengi chini yake na sisi tulikuwa hatukamati wanunuzi tunakamata wale wanaowauzia.”
Lyimo alisema moja ya sababu za mafanikio hayo ni serikali kuongeza vifaa vya kisasa, rasilimali fedha na rasilimaliwatu katika DCEA.
“Kifaa kimoja kinauzwa Shilingi milioni 200, bila hivyo tusingemudu kukamata mitandao yote hiyo, vifaa vinarahisisha unakamata watu bandarini au kiwanja cha ndege unapima ndani ya sekunde mbili au tatu… kuna kifaa kimoja kinapima dawa za kulevya aina 12,000 hicho sio mchezo,” alisema.
Lyimo alisema jambo lingine walilofanikiwa ni kuanzishwa kwa kanda tano zilizowapa urahisi wa kufanya msako wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya zikiwemo heroini, kokeni, bangi na mirungi.
Alitaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa vituo vya kutibu wenye uraibu kufikia 16 kutoka 11 vya awali.
“Vinafanya kazi waraibu 18,170 wanahudumiwa… na bado kuna vituo vitano vinajengwa kwa mara moja, viwili vimekamilika bado tunasubiri vitatu vinajengwa,” alisema.



