Waziri Kombo awasili Vietnam

VIETNAM : WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Mahmoud Thabit Kombo , amewasili jijini Hanoi kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Katika ziara hiyo, Waziri Kombo ataongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali ya Vietnam, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi.
Mazungumzo hayo yanalenga pia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya mataifa haya mawili.
Aidha, mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuongeza masoko ya bidhaa za kilimo na uvuvi kutoka Tanzania, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika uwekezaji, viwanda na teknolojia.

Ujumbe wa Tanzania utajumuisha viongozi na watendaji wa Serikali na sekta binafsi, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Gilead Teri, pamoja na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, akiwemo Balozi John Ulanga na Felista Rugambwa.
Tanzania na Vietnam zina uhusiano wa kihistoria ulioimarisha biashara baina yao, ambapo mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Vietnam yameongezeka kwa asilimia 38 kati ya mwaka 2020 na 2024.
Vietnam pia imewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zenye thamani ya USD bilioni 2.362, na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 226,000.
SOMA: Balozi Kombo atakuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 27 ya CFR



