Makonda: Najivunia Makalla kunirithi uenezi

ARUSHA: MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema Makalla alimshika mkono alipopeleka wazo la kuanzisha matawi ya vyuo vikuu nchi nzima na kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinaimarika, hivyo ni fahari kwake kurithiwa na mtu wa aina yake katika nafasi hiyo ya uenezi na ni heshima kubwa kwani anakijua vizuri chama na mifumo ya serikali.
Makonda ameeleza hayo leo Juni 5, wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Mto wa Mbu Wilaya ya Monduli mkoani Arusha wakati Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla akisalimia wananchi hao akielekea Karatu kuendelea na ziara yake katika mikoa ya Kaskazini.
“Mimi nimetoka kwenye nafasi ya kaka angu Makalla huyu ni mlezi wangu wakati nasoma chuo cha Ushirika Moshi yeye ndi alikuwa muweka hazina mkuu wa CCM na katibu Mkuu alikuwa Mzee Yusuph Makamba tulikuwa tunaenda kama vijana makada tunapeleka proposal kama Makalla alinishika mkono,” amesema Makonda.
Katika hatua nyingine Makonda amesema serikali inafanya juhudi kutengeneza mazingira bora zaidi ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo nchi.
Ameeleza hayo akitaja mradi wa Magadi Soda wa Enguruka wilayani Monduli ambao unatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh trilioni mbili hadi kukamilika kwake lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hiyo ya madini yatakayopata soko ndani na nje ya nchi.
Pia Makonda amewaomba wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo kwani ni msingi wa shughuli za maendeleo na uchumi na ikitoweka hakuna kitakachoweza kufanyika.

