Ukosefu wa fedha watajwa kuua taasisi za vijana

DAR ES SALAAM: Ukosefu wa fedha, masharti magumu kutoka kwa wafadhili, kutokuwa na maarifa ya kutosha ya uendeshaji wa taasisi na rasilimali zake ni miongoni mwa changamoto zinazochangia taasisi nyingi zinazoanzishwa na vijana kufa kabla ya kufikia malengo yake.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Her Initiative, Lydia Charles, katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya uongozi kwa taasisi 20 zinazoongozwa na vijana kupitia programu ya Adaptive Leadership Program chini ya mradi wa Ustawi Lab.
Amesema changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wanaotamani kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia taasisi zao, jambo lililowasukuma kuanzisha mafunzo hayo ya uongozi ili kuwajengea uwezo wa kimfumo na kimkakati.

“Tuliona kuna haja ya kuimarisha uwezo wa viongozi vijana kwa kuwapatia mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali, kuboresha mifumo ya taasisi zao na kuzifanya zidumu kwa muda mrefu,” amesema Lydia.
Ameongeza kuwa katika dunia ya sasa yenye mabadiliko ya kasi katika teknolojia, siasa na uchumi, viongozi vijana wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na kasi ya mabadiliko na kuyageuza kuwa fursa za maendeleo.
Aidha, Lydia ameitaka Serikali kuweka mikakati rafiki kwa vijana wanaoanzisha mashirika, ikiwemo urahisishaji wa usajili, masuala ya kodi na kuwepo kwa mifuko maalum ya ruzuku kwa mashirika yanayoongozwa na vijana.“Tunaamini ndoto za vijana wa Tanzania hazitakufa, bali zitang’ara,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Uholanzi, Chikulupi Kasaka, alieleza kuwa moja ya sababu zinazofanya baadhi ya taasisi kukosa ufadhili ni kukosekana kwa sera na muundo wa kiuendeshaji ulio imara.
“Wengine huendesha taasisi kwa misingi ya undugu au urafiki badala ya kitaaluma, huku wakiwa hawana idara rasmi za utekelezaji,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya mashirika hayana uwezo wa kusimamia fedha wanazoomba, jambo linalowafanya wafadhili kuingiwa na mashaka kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali hizo.
Pia amebainisha kuwa mabadiliko ya kimataifa yanayoathiri uchumi wa nchi wahisani yamesababisha kupungua kwa ufadhili, na hivyo mashirika ya vijana yanapaswa kujiimarisha na kuandaa miradi ya muda mrefu yenye matokeo ya moja kwa moja kwa jamii, badala ya kutegemea mikutano ya siku chache isiyo na tija ya kudumu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi, aliwataka vijana kuwa wabunifu, kufuata sheria na maadili, huku wakitumia fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Uaminifu na matumizi sahihi ya fedha ni msingi wa kudumu kwa taasisi yoyote. Tufanye kazi kwa bidii na kwa kujituma ili kuleta mabadiliko chanya kwa taifa,” amehitimisha.



