Myenzi atangaza nia ya ubunge Kilolo

IRINGA: ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Comrade Kilian Edson Myenzi, ametangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kilolo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, akiahidi kusukuma maendeleo ya kijani kwa kasi kubwa huku akieleza kwa uchungu changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa leo, Myenzi amesema kuwa licha ya kazi kubwa na ya kupongezwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, bado kuna uhitaji wa kuwa na mwakilishi mwenye dira, mchapakazi na anayewasiliana moja kwa moja na wananchi wa Kilolo.
“Kilolo ni hazina iliyojificha – tuna rasilimali watu, ardhi ya kutosha, misitu, vyanzo vya maji na hata madini. Lakini bado hatujayaweka haya kwenye ramani ya kitaifa ipasavyo kwa sababu ya miundombinu mibovu na masoko duni,” amesema Myenzi.
Kwa uchungu, alieleza kuwa maeneo mengi ya Kilolo hayaipitiki nyakati za mvua, jambo linalokatisha tamaa wakulima na wawekezaji.
Akapendekeza mkakati wa kujenga barabara za zege katika maeneo korofi badala ya kungoja miradi mikubwa ya muda mrefu ambayo haijafika vijijini kwa kasi inayohitajika.
SOMA ZAIDI
“Tutashauriana na Serikali kujenga barabara imara na rahisi – ili mazao ya chai, parachichi, matunda na mboga yafike sokoni haraka. Kilolo inaweza kuwa ‘Green Gold Zone’ ya Tanzania,” alifafanua.
Myenzi ambaye amekuwa kiongozi kijana wa mfano ndani ya chama, aliahidi kuwa mstari wa mbele katika kutafuta masoko ya nje kwa mazao ya Kilolo kwa kushirikiana na wizara husika na sekta binafsi, akisema uchumi wa eneo hilo utaongezeka kwa kasi ya 5G ikiwa tutabadilika na kwenda na wakati.
Aidha aligusia barabara ya Ipogolo, Idete hadi Mgeta mkoani Morogori akisema ataipigia debe ili itengenezwe na kuwa ya kupitika kwa mwaka mzima.

