CCM yasogeza mbele uteuzi wa Wagombea 2025

Hii ni tofauti na ratiba ya awali iliyotangazwa kupitia taarifa ya Aprili 10, 2025.
Katibu Mkuu CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi

DODOMA – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kusogeza mbele ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, baada ya kupitia ushauri kutoka kwa wanachama wake.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, mchakato huo sasa utaanza rasmi Juni 28, 2025 saa 2:00 asubuhi na utakamilika Julai 2, 2025 saa 10:00 jioni. Hii ni tofauti na ratiba ya awali iliyotangazwa kupitia taarifa ya Aprili 10, 2025.

“Chama kimefanya maamuzi haya baada ya mashauriano na wanachama wake, kutafakari kwa kina na kupima ushauri uliotolewa kwa makini. Tunawahakikishia wanachama wetu kuwa ratiba mpya itazingatia utaratibu ule ule uliotangazwa awali,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Advertisement

Taarifa hiyo imeendelea kusisitiza kuwa mchakato huo utaendeshwa kwa misingi ya haki, uwazi na kufuata kanuni na miongozo ya chama, huku chama kikieleza dhamira yake ya kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza demokrasia ya ndani na kuhakikisha wagombea wanaopitishwa wanakidhi matarajio ya Watanzania.

Uamuzi huu unakuja wakati nchi ikijiandaa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, huku CCM ikisisitiza kuwa itaendelea kuwa imara na kuongoza kwa mujibu wa maadili na misingi ya kuasisiwa kwake.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *