TAMWA yamkabidhi uenyekiti Dk Kaale

DAR-ES-SALAAM : CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepata Mwenyekiti mpya wa Bodi, Dk Kaanaeli Kaale, ambaye atakiongoza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, akichukua nafasi ya Joyce Shebe aliyemaliza muda wake baada ya kulitumikia chama hicho kwa miaka sita mfululizo.
Dk Kaale alichaguliwa katika Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa chama hicho uliofanyika Juni 28, jijini Dar es Salaam, ambapo pia wajumbe wengine sita wa Bodi walipatikana.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Dk Kaale amesema atajikita katika kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na uongozi uliopita, huku akiahidi kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuwafikia wanachama wote, wakiwemo walioko pembezoni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto za upatikanaji wa taarifa.
“Tutaendeleza yote yaliyofanywa na bodi iliyopita. Kila kitabu kina zama zake. Tutatumia fursa za TEHAMA kuwajumuisha wote waliopuuzwa au kusahaulika kutokana na changamoto za kiteknolojia,” alisema Dk Kaale.
Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa uchaguzi, ni muhimu kwa wanahabari wanawake kuandika habari zenye maadili, zinazohamasisha amani na haki, huku akiwahimiza kukemea udhalilishaji wa wanawake wanasiasa kupitia mitandao ya kijamii.
“Tujitahidi kuhakikisha wanawake wanashika nafasi za juu za uongozi na maamuzi ili kufikia angalau asilimia 50 ya ushiriki wa wanawake, ambayo ni miongoni mwa malengo ya TAMWA,” alisisitiza.
SOMA: Hongera Tamwa, TCRA, asante Rais Samia
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya TAMWA, Joyce Shebe, aliwashukuru wanachama kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha uongozi, huku akieleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake.
Alisema chama hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kimefanikiwa kuzindua Tuzo za Samia Kalamu, zinazolenga kuimarisha taaluma ya habari, kuhamasisha uzalendo na kuhimiza maendeleo.
Aidha, Shebe alibainisha kuwa chama hicho kiliadhimisha miaka 36 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, tukio lililosaidia kukitangaza zaidi chama na kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali wa maendeleo.
“TAMWA pia kimefanikiwa kukarabati jengo lake lililopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, kuwekeza katika shamba la Kibaha pamoja na kuendesha programu mbalimbali za kijinsia,” alisema.
Shebe aliwahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika uchaguzi si kwa kupiga kura tu bali kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, huku akivitaka vyama vya siasa kusimamia utekelezaji wa sera za kijinsia ndani ya vyama vyao.
Katika uchaguzi huo, pamoja na Dk Kaale, wajumbe wengine waliochaguliwa kuingia kwenye Bodi ya TAMWA ni Dk Mary Kafyome, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma; Kulthum Ally, Mwanahabari Mwandamizi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN); na Asha Abdi kutoka Zanzibar.
Wajumbe wengine ni CPA Caroline Mdundo (mshauri wa masuala ya fedha), Wakili Annuciater Bulashi (mshauri wa masuala ya kisheria) na Dk Stella Ng’oma (mshauri wa masuala ya kijamii).
Katika mkutano huo, wanachama wapya 117 kutoka Tanzania Bara walipitishwa pamoja na wanachama watano kutoka Zanzibar.
TAMWA imeendelea kuwa chombo muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia na kusimamia haki za wanawake na wasichana kupitia taaluma ya uandishi wa habari na sera za maendeleo jumuishi.



