Mwankenja aomba kura, aahidi kuijenga Lupa

Mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Lupa, Geofrey Mwankenja, amewaomba wajumbe wa CCM kumpa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akiahidi siasa safi na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote wa Lupa.
Mwankenja, kada msomi na mfanyabiashara wa madini, aliteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kuwania nafasi hiyo katika mchakato wa kura za maoni.
Uteuzi wake umetajwa na wachambuzi wa siasa kuwa ni sehemu ya muelekeo wa chama hicho kutoa nafasi kwa viongozi wenye weledi, maono na uhusiano wa karibu na wananchi.
Akizungumza katika mikutano ya ndani na wajumbe wa CCM maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, Mwankenja alisema anauchukulia uteuzi huo kwa unyenyekevu mkubwa na kama fursa ya kweli ya kuwatumikia wananchi waliomlea na kumuamini.
Alisema anatambua changamoto zinazowakabili wakazi wa Lupa kwa kuwa alizipitia akiwa mtoto, akiishi katika familia ya wakulima.
Aliainisha maeneo ya vipaumbele endapo atapewa ridhaa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji safi na salama kwa kuchimba visima na kuimarisha usambazaji wa maji, kuboresha barabara zinazounganisha kata na vijiji ili kurahisisha usafiri na usambazaji wa huduma muhimu, kuweka mazingira ya vijana kujiajiri kwa kuanzisha vituo vya mafunzo ya ufundi pamoja na kutoa mikopo rafiki kwa wajasiriamali chipukizi
Mengine ni kuboresha mazingira ya shule, vifaa vya kujifunzia na kuongeza motisha kwa walimu, sambamba na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya hasa katika maeneo ya pembezoni mwa jimbo hilo.
Baadhi ya wakazi wa Lupa waliomzungumzia Mwankenja, wamemwelezea kama kiongozi mwenye maono, anayejali watu na ambaye hana kiburi wala majivuno.
Walisema wameshuhudia mchango wake hata kabla hajawa mgombea, na sasa wana matumaini makubwa kwamba atakuwa sauti ya mabadiliko chanya kwa jamii.
Waliongeza kuwa uteuzi wa Mwankenja umeongeza ari miongoni mwao kwa kuwa ni mtu anayeelewa changamoto zao na ambaye amekuwa nao bega kwa bega hata kabla ya siasa.
Mwankenja pia aliwataka wanachama wa CCM na wafuasi wake kushiriki mchakato wa kura za maoni kwa amani na heshima, akisisitiza kuwa siasa za matusi na chuki hazina nafasi katika kizazi cha sasa.
Alisema ushindani wa kweli unatakiwa kuwa wa sera, maono na uwezo wa kuleta mabadiliko.
“Uongozi siyo kupambana kwa maneno, bali ni kushindana kwa mipango na vitendo. Mimi nipo tayari kusikiliza, kujifunza na kushirikiana na kila mmoja kwa ajili ya Lupa yenye neema,” alisema.
Mbali na Mwankenja, wengine waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM kuwania ubunge Jimbo la Lupa ni Noel Damson Nthangu, Masache Njelu Kasaka na Sara Joel Sompo.

