Serikali Mtandao wapongezwa kuchangia mapinduzi kilimo

DODOMA; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Athumani Kilundumya, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuchangia mapinduzi katika sekta ya kilimo kupitia mifumo ya kidigitali iliyobuniwa na mamlaka.
Kilundumya ameyasema hayo jana mara baada ya kutembelea banda ya Mamlaka ya Serikali Mtandao wakati wa Maonesho ya 32 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane 2025) ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema kazi kubwa iliyofanywa na Mamlaka hiyo kwa kujenga mifumo kumechangia mageuzi ya kilimo ya kidigitali Kilundumya alisema kuwa, Wizara ya Kilimo imeshuhudia jitihada mbalimbali zinazofanywa na e-GA katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya sekta ya kilimo ili kuimarisha sekta hiyo.
“Natambua jitihada za e-GA ikiwemo ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa mbolea kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) ambao unawezesha usajili na utoaji wa leseni kwa wauzaji na wasambazaji wa mbolea, utambuzi wa maghala ya utunzaji wa mbolea pamoja na udhibiti wa soko la mbolea.”
Alisema kuwa, kupitia mfumo huo Serikali inaweza kudhibiti soko la mbolea na kuhakikisha mbolea inauzwa kwa bei rafiki kutokana na ruzuku ya Serikali katika mbolea na hivyo wakulima kuweza kulima na kupata faida.
Aidha, Kilundumya alizitaja taasisi nyingine zilizoshirikiana na e-GA katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kuwa ni pamoja na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa kujenga Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushiriki na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kujenga Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Umwagiliaji.
“Nafahamu kuna Mfumo wa eKilimo ambao unarahisisha utendaji kazi katika sekta ya kilimo natamani kuona baadaye mfumo huu ukituwezesha kupata taarifa za wakulima wote hata wale wadogo waliopo vijijini ambao hawajasajiliwa, ni Imani yangu Wizara tukileta mahitaji haya e-GA mtayafanyia kazi.”
Naye Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amemshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea banda la e-GA na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa sambamba na kuendeleza ushirikiano wa e-GA na sekta ya kilimo katika kuimarisha TEHAMA katika taasisi hiyo.
Alisema kuwa, e-GA imekuwa mstari wa mbele katika kutengeneza bunifu za mifumo ya kimkakati kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi ya kidijitali kwa jamii ya mijini na vijijini.
Maonesho ya kitaifa ya nanenane ,mwaka 2025 yanafanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.