Wasioripoti JKT waongezewa siku nne

DODOMA; JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetoa fursa nyingine ya siku nne kwa vijana ambao bado kuripoti kwenye makambi waliyopangiwa kufanya hivyo katika kambi yoyote iliyokaribu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Tawi la Oparesheni na Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani wakati wa kutoka taarifa kwa umma kuhusu wito wa kuripoti makambini kwa vijana waliochanguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria mwaka 2026.

Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele alitoa wito kwa vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026, kuhudhuria Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.

Sanjari na wito huo, JKT liliwapangia makambi ya kwenda kupatiwa mafunzo vijana hao na walitakiwa kuripoti katika makambi ya JKT  kuanzia Juni mosi hadi Juni 7 mwaka huu.

Brigedia Jenerali Mnyani alisema: “Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele anawataka vijana wote waliochaguliwa na wakashindwa kuripoti katika makambi ya JKT waliyopangiwa kutokana na sababu mbalimbali, kwenda kuripoti katika makambi ya JKT yaliyokaribu na maeneo wanayoishi.”


Hata hivyo alisema vijana hao hawapaswi kwenda kwenye makambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani, Kambi ya Makutupora JKT iliyopo mkoani Dodoma na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT), kilichopo Kimbiji jijini Dar es Salaam.

“Vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia leo Juni 12, 2026 hadi Juni 15, 2026 bila kukosa ili waweze kujiunga na mafunzo hayo muhimu ya kujenga uzalendo, nidhamu na stadi mbalimbali za maisha,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button