Askofu: Tukatae rushwa Uchaguzi Mkuu

TANGA : KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki limetoa wito kwa wananchi kukataa rushwa za wagombea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Askofu wa dayosisi hiyo, Msafiri Mbilu alisema hayo katika ibada ya kumuingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kaskazini la Dayosisi hiyo, Mchungaji Charles Kakai. Ibada hiyo ilifanyika katika Usharika wa Mlalo wilayani Lushoto Mkoani Tanga.

“Tuendelee kumgeukia Mungu tu na tumuombe hata katika Uchaguzi Mkuu ulio mbele yetu, atuchagulie viongozi wazuri wenye nia ya kuongoza taifa letu. Nitoe wito kwa wanadayosisi wote tusikubali kurubuniwa kwa kupewa rushwa, rushwa ni adui wa haki.

Eti kura yangu niiuze, ninunuliwe mimi, hapana, usikubali kuuza kura yako,” alisema Askofu Mbilu. Aliongeza: “Kampigie kura yule unayemtaka, yule unayeona atatuvusha kweli, huyo anafaa na ukiona hafai usimpe hata kama ni jirani yako, maana hatuchagui kwa ajili ya ndugu zetu, tunachagua viongozi watakaolivusha taifa hili”.

Askofu Mbilu alisema viongozi watakaochaguliwa si wa kuongoza familia bali wataongoza eneo kubwa la nchi hivyo wapiga kura wazingatie kuchagua wenye kuliletea maendeleo taifa na jamii. “Mimi sishawishi mchague nani, maana hata mimi ninajua nitampa nani kura yangu na silazimishwi na mtu kumchagua yeyote na wewe fanya vivyo hivyo hata kama ni mume wako, ukiona hataleta maendeleo yoyote usimpe kura,” alisema.

Awali, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Julius Madiga alisema Aprili 5 mwaka huu, Halmashauri Kuu Dayosisi hiyo ilifanya kikao maalumu kilichofanyika Magamba, Lushoto. Madiga alisema kikao hicho kilizungumzia uchaguzi wa wakuu wa majimbo na kwa kuzingatia katiba ya dayosisi hiyo, halmashauri kuu ilimchagua Mchungaji Kakai kuwa Mkuu wa Jimbo. Baada ya kuingizwa kazini, Mchungaji Kakai aliwashukuru viongozi walioona anafaa kutumika kwa nafasi hiyo na ameahidi kutimiza wajibu huo kwa kujitoa na kuendeleza kazi ya Mungu kwa uaminifu.

Alisema maono yake ni kueneza injili na mafundisho sahihi ya neno la Mungu kwa watoto, wanawake, wanaume, vijana na familia Wakristo wapate msingi imara wa neno na Mungu. Alitaja vipaumbele vyake vingine ni kuelimisha jamii masuala ya kijamii, kiuchumi ili waumini wajikwamue kiuchumi. Pia, ameahidi kuendeleza ushirikiano na serikali katika kuijenga jamii kimaadili.

Hapo awali nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Mchungaji Anderson Kipande. SOMA: Viongozi wa dini watakiwa kuepuka uchochezi uchaguzi mkuu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button