Kabudi ahimiza uzalendo Uchaguzi Mkuu

DAR-ES-SALAAM : SERIKALI imeagiza waandishi wa habari waandike habari za Uchaguzi Mkuu wakizingatia uzalendo badala ya masilahi binafsi. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi pia aliagiza waandishi wa habari waandike habari za uchaguzi zenye masilahi ya taifa na wajiepushe na vitendo vya rushwa.

Profesa Kabudi alisema hayo Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na wadau wengine wakiwemo maofisa wa polisi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu. SOMA: Waandishi watakiwa kuithibitishia dunia Tanzania ni nchi ya amani

“Watanzania watangulize uzalendo mbele, hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, tuhakikishe uchaguzi unakuwa wa amani na wanahabari zingatieni misingi ya taaluma kuweni wazalendo, uchaguzi uwe wa amani,” alisema.

Profesa Kabudi alihimiza vyombo vya habari vieleze sera za vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi na si kuandika habari za uchochezi. “Tumieni vyombo vyenu vya habari kuandika habari za kujenga na epukeni masilahi binafsi ambayo hayana tija kwa umma,” alisema.

Profesa Kabudi alitaka Jeshi la Polisi lishirikiane na vyombo vya habari kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa usalama na amani na kila mmoja atambue majukumu na mipaka yake. Alisema sekta ya habari inatakiwa kutimiza mambo matano ambayo ni kuwajulisha wananchi kuhusu haki na wajibu, kuelimisha sera za wagombea, kuibua na kufuatilia ukiukwaji wa sheria, kuhamasisha ushiriki wa makundi maalumu na kupambana na taarifa potofu, uzushi na kutoshiriki kuzisambaza.

Profesa Kabudi alisema ili kutekeleza mambo hayo ni muhimu kuheshimu taaluma na maadili ya uandishi wa habari, ambayo alisema ni wajibu wao kuyafuata na kuyaheshimu, kwa kuwa kutofanya hivyo ni kosa kisheria. “Jiepusheni na habari za uchochezi, upendeleo na uzushi zinazolenga kuharibu heshima, hadhi ya mtu au taasisi, timizeni wajibu wenu wa kutoa fursa kwa wagombea wote kwa usawa,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button