Samia atangaza neema kilimo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema serikali yake bado ina uwezo wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo.

Mgombea wa urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan amesema hayo alipohutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Mlima wa Reli uliopo katika Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya.

Samia amesema ruzuku ya pembejeo za kilimo zinatolewa kwa wakulima wote ili kuongeza wigo wa uzalishaji
wa mazao. Amehimiza wakulima waendelee kujisajili katika mfumo ili wapate mbolea na mbegu za ruzuku.

“Bado uwezo wetu wa kutoa ruzuku zaidi upo, wakulima mjisajili na mtunze namba zenu za siri. Mbolea, mbegu na pembejeo tunazotoa kwa ruzuku si kwa ajili ya kuuzwa, msishirikane na waovu kuziuza, tunatoa kwa ruzuku kwa sababu serikali inabeba gharama kwa ajili ya Watanzania ili wazalishe na si kufanyia biashara,” amesema Samia.

SOMA: CCM yatumia kete tatu kupata ushindi

Amesema serikali yake ilifanyia kazi ombi la wakulima wa Mkoa wa Mbeya walilotoa mwaka 2022 kuomba mbolea ya ruzuku na sasa imekuwa ikitoa mbolea, mbegu na pembejeo nyingine kwa ruzuku kwa wakulima nchi nzima.

“Nilikuja hapa Mbalizi Agosti 5, mwaka 2022 miongoni mwa vitu mlivyonieleza ni kuwa ninyi ni wakulima wa pareto, mahindi, kahawa, viazi na mazao mengine madogo madogo lakini hitaji lenu kubwa kwa wakati ule ilikuwa ni mbolea, tena mbolea ya ruzuku,” amesema Samia.

Ameongeza: “Nataka kuwaambia tangu nilipotoka pale tumefanyia kazi na mbolea ya ruzuku inagawiwa si tu kwa Mbalizi au Mbeya inagawiwa kwa wakulima nchi nzima, kila maeneo kuna mbolea za ruzuku.”

Samia amesema serikali imekwenda mbali zaidi kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa kila zao ikiwamo mahindi, mpunga, tumbaku na parachichi.

“Kila zao lina mbolea yake ya kupandia na kukuzia na mbolea zote hizi tunazitoa kwa ruzuku, mbegu bora tunazitoa kwa ruzuku, lengo letu Tanzania izalishe kama ilivyo sasa lakini tuuze kwa nchi jirani kwa sababu kwa sasa hakuna mazao ya biashara wala mazao ya chakula yote ni mazao ya biashara, Tanzania tunauza sana nje kupitia mazao ya kilimo,” amesema.

Aidha, akiwa Mlowo mkoani Songwe njiani kwenda Mbeya, Samia amesema serikali itafungua vituo vya kununua mahindi kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Kwa upande wa wafugaji amesema serikali itakamilisha ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa Utengule. Pia, amesema serikali inaendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo yenye lengo la kuongeza hadhi ya mifugo kutoka Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Nendeni kachagueni wagombea wa CCM kwa mafiga matatu yaani nafasi ya rais, ubunge na madiwani. Na
mama yenu msinisahau niko hapa, mama wa maendeleo, mama wa matumaini mkanimiminie kura tuje tufanye kazi,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button