Chaumma kubadili mifumo ya kodi, kupunguza VAT
CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeahidi kukuza uchumi kwa kubadili mifumo ya kodi.
Ilani ya uchaguzi ya chama hicho 2025-2030 imeeleza kuwa serikali ya chama hicho itatunga upya sera na sheria za kodi ili viendane na uhalisia wa kipato cha Mtanzania mmoja mmoja.
Chaumma imeahidi kuanzisha bodi ya pamoja ya kodi ili kudhibiti kodi, kuchapisha orodha ya tozo na kodi zinazoruhusiwa na kutangaza kodi nyingine zote zisizotajwa kuwa haramu.
Chama hicho kimeeleza serikali ya chama hicho itaboresha sekta ya biashara kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kupunguza baadhi ya kodi, ushuru na tozo.
Ilani imeeleza Chaumma itapunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 ya sasa hadi asilimia 12.
SOMA: Chaumma yaahidi mshahara 800,000, mchele kilo Sh 500
Chaumma imeeleza ili kuboresha mazingira na sheria ipo haja ya kufanya majadiliano kati ya serikali na wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi na kushughulikia tatizo la rushwa.
Chama hicho kimeahidi kufuta ushuru wa bidhaa uliowekwa kwenye bidhaa na huduma muhimu ili kumpunguzia gharama za maisha mwananchi.
Ilani imeeleza Chaumma itafuta VAT kwenye pembejeo na bidhaa zote za chakula ikiwemo sukari, mafuta, ngano, mchele, nyama na nyinginezo ili kumwezesha mwananchi kupata chakula kwa bei nafuu.
Chama hicho kimeahidi kuwa na viwango rafiki vya kodi ili kuhamasisha ulipaji wa kodi na hivyo kupunguza tatizo la ukwepaji kodi.
“Kesi za ukwepaji kodi lazima zifunguliwe dhidi ya wakwepaji, vinginevyo umma hautaheshimu sheria za kodi, pia sheria za kodi za Tanzania zinajulikana kwa utata wake. Ni muhimu sheria za kodi ziwe rahisi kueleweka kwa watu wote; inapaswa kuelezwa kwa lugha nyepesi, wazi na inayoeleweka,” imeeleza ilani hiyo.
Chaumma imeeleza ni wakati mwafaka kwa teknolojia ya kompyuta kwenda sambamba na utashi wa kisiasa ili kutekeleza ukusanyaji wa kodi kikamilifu na kuleta mapato makubwa zaidi kwa Tanzania.
Chama hicho kimeahidi kukuza uchumi katika sekta ya biashara kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kupunguza baadhi ya kodi, ushuru na tozo ili kuvutia mitaji kwa ajili ya biashara.
Ilani ya chama hicho imeahidi kuondoa usumbufu wa kikodi kwa wafanyabiashara kwa kuwaruhusu watoe mizigo mipakani, bandarini na viwanja vya ndege baada ya kujulikana kodi yao ni kiasi gani na ndani ya siku 14 baada ya kutoa mizigo wawe wamelipa kodi yote.
Chaumma imeahidi kuwatambua wafanyabiashara wa kati na wadogo ili kuwawekea mazingira ya kuwa na kodi rafiki na kulinda mitaji yao.
Pia, chama hicho kimeahidi kuwapa mikopo na yenye masharti nafuu vijana na wanawake wanaotaka kuanzisha biashara na kutakuwa na dirisha la mikopo kwenye kila halmashauri.
Chama hicho kimeahidi kuweka sera za kulinda bidhaa za ndani dhidi ya uingizwaji wa bidhaa za nje zisizo na ubora, itapunguza na kufuta baadhi ya kodi, tozo na ushuru ambazo hutozwa na wakala na taasisi za serikali kwenye biashara zinazofanyika nchini.


