Serikali yalifungua Ziwa Ikimba, samaki kuongezeka

KAGERA: Serikali imelifungua Ziwa Ikimba lililopo Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera ikiwa ni miezi 6 tangu ilipolifunga kwa lengo la kuongeza kiwango cha samaki.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufungua ziwa hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amewataka wananchi wanaonufaika na uvuvi wa ziwa hilo kutoacha shughuli Ilizokuwa zikiwaingizia kipato wakati ziwa lilipokuwa limefungwa ili kuwa na uchumi jumuishi kwenye eneo hilo.
“Niwapongeze sana kwa kutii makubaliano ya kutofanya shughuli za uvuvi katika kipindi chote cha ufungaji wa ziwa na leo sote tumeshuhudia matunda ya uvumilivu wenu kwa kipindi cha miezi 6 niombe muendelee kutunza ziwa hili lakini tusiache shughuli nyingine pia tufanye shughuli zote ili kuinua uchumi wetu kwa vyanzo tofauti tofauti,” alisema Sima.

Alisema kuwa ufunguzi wa ziwa hilo utaongeza mapato ya halmashauri ambapo mpaka sasa takribani Sh miliioni 8 zimeshapatikana kupitia usajili wa mitumbwi ya kuvulia samaki pekee ambapo tani 15 kwa mwaka zitaongeza mapato makubwa ya halmashauri hiyo ambapo amedai kuwa ni vyema wavuvi wanaweka utaratibu wa kuwa wanapumuzisha ziwa hilo ili kuongeza samaki .
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede amesema kuwa Wizara ya Uvuvi itaendelea kuchagiza shughuli za uvuvi kwenye ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uvuvi unaokubalika kisheria na kuongeza takribani vifaranga milioni 1 vya samaki kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu.
“Wataalam wetu wa Wizara wataweka kambi hapa kwa ajili ya kutoa elimu hiyo lakini pia watakaa na nyie darasani kabisa ilo kuelimishana kuhusu uvuvi unaofaa na tutaongeza tena vifaranga katika ziwa hili ,” alisema Mhede.

Akielezea hali ya upatikanaji wa samaki ilivyo hivi sasa kwenye ziwa hilo, Mkurugenzi wa Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kitaalam uliofanyika leo ziwani hapo, kiwango cha mavuno ya samaki kwa mwaka kinatarajia kupanda kutoka tani 1.5 hadi kufikia tani 15 huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka zaidi endapo rasilimali za uvuvi zilizowekwa ziwani humo zitalindwa kikamilifu.
“Huu ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka, wananchi wanapata tija na mapato ya Serikali kupitia sekta ya Uvuvi yanaongezeka,” alisema Prof. Sheikh.
Wavuvi wanaonufaika na ziwa hilo Enickson Charles na Rehema Hamza wamesema kuwa kufunguliwa kwa ziwa hilo na kiwango cha samaki wanaopatikana ni fursa ya wao kukuza uchumi wao kupitia maji hayo ambapo wameongeza kuwa watahakikisha wanalinda rasilimali hizo ili zisitoweke tena kama ilivyokuwa awali.
Ziwa hilo lilifungwa Machi 12,2025 kwa makubaliano ya hiyari baina ya Serikali, wavuvi na wananchi wanaonufaika na ziwa hilo kwa lengo la kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki ili kukuza uchumi wa kwa wakazi wa eneo hilo, mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla.



