Senyamule aita wawekezaji hoteli nyota 5 Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amezialika sekta binafsi mkoani humo kuwekeza katika sekta ya hoteli kwa kujenga za nyota tano ili kuvutia mikutano ya kimataifa kufanyika jijini humo.

Licha ya Dodoma kuwa makao makuu ya serikali, lakini hakuna mikutano mikubwa ya kimataifa inayofanyika.

Hiyo ni kutokana na kukosekana kwa hoteli za hadhi kubwa, zikiwemo zenye hadhi ya nyota tano.

SOMA: Dodoma tayari kwa mabalozi, serikali yatoa viwanja bure

Senyamule amesema hayo jijini hapa wakati akizungumza na wamiliki wa hoteli wa Mkoa wa Dodoma na kuhamasisha watu wa sekta binafsi kuwekeza katika kujenga hoteli za hadhi hiyo, ili kuvutia mikutano mikubwa ya kimataifa kufanyika jijini humo.

“Nitoe mwito kwa wawekezaji kuwekeza hoteli zenye hadhi ya nyota tano au mziboreshe zilizopo hivi sasa. Ili ziweze kufikia hadhi hiyo, serikali imefanya uwekezaji mkubwa, ikiwamo ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato,” amesema.

Ameongeza: “Hoteli zenye hadhi ya nyota tano zisizopungua tano zinatakiwa, ili tuwe na hadhi ya kufanya shughuli hizo za kimataifa katika eneo husika. Hivyo, natoa mwito wawekezaji kutumia fursa hiyo”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Hoteli Mkoa wa Dodoma, Gabriel Mauna alizipongeza mamlaka za maji na umeme kwa kufanya maboresho katika sekta zao na kurahisishwa huduma hizo muhimu.

“Tunashukuru serikali ya mkoa, kwa sababu mara ya mwisho tulipokutana tulitoa changamoto zetu na mojawapo ilikuwa ni umeme na maji. Tunashukuru changamoto hizi zimefanyiwa kazi,” amesema Mauna.

Mkuu wa Mkoa alikutana na wamiliki wa hoteli mkoani humo, ukiwa ni mwendelezo wa vikao kazi vyake vya kuzungumza na makundi tofauti ya kijamii na dhamira kuu ikiwa ni kuzungumzia ajenda mbalimbali pamoja na kusikiliza kero zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button