RUCU kujadili nafasi ya ubia Dira ya Maendeleo 2050

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano kubwa la kitaaluma litakalofanyika Septemba 9 katika Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), likihusisha zaidi ya washiriki 500 kutoka sekta mbalimbali nchini.

Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya RUCU na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), likiwa na dhamira ya kuchambua mchango wa ubia huo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Afisa Mahusiano wa RUCU, Mauna Belius, amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa la kitaaluma na kimkakati la kujadili namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Tutabadilishana uzoefu wa kitaifa na kimataifa kuhusu miradi ya ubia, sambamba na kutoa mapendekezo ya sera za kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi,” alisema Belius.

Miongoni mwa vivutio vikubwa vya kongamano hilo ni mjadala wa kitaaluma utakaongozwa na mwanahabari nguli, Tido Mhando, huku taasisi zaidi ya 100 zikitarajiwa kushiriki.

Belius aliongeza kuwa maandalizi yote yamekamilika na kongamano hilo litaonyeshwa mubashara kupitia vyombo vya habari ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Tunawaalika wakazi wa Iringa na maeneo jirani kushiriki, kwani hii ni fursa adimu ya kujifunza na kuchangia mawazo katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa,” alisisitiza.

RUCU imeendelea kujijengea heshima kama kitovu cha mijadala ya kitaaluma na utafiti, na kongamano hilo limeelezwa kuwa sehemu ya juhudi zake za kuchochea maendeleo kupitia maarifa na ubunifu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button