Ngajilo: Iringa ni mkoa wa madini, wananchi wanapaswa kunufaika nayo

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Fadhili Ngajilo, amesema Mkoa wa Iringa umebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini, na sasa ni wakati wa kuhakikisha wananchi wenyewe wanashiriki moja kwa moja katika uchimbaji na biashara ya madini hayo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kihesa, Ngajilo alisema:

“Nikiwa mbunge, nitazungumzia suala la madini kwa nguvu zote. Iringa ni mkoa wa madini, lakini halijazungumzwa vya kutosha.

“Taarifa za madini zipo ofisi ya madini. Mkoa huu umebarikiwa madini kila mahali — dhahabu, kopa, makaa, udongo wa tiles — lakini wananchi hawajanufaika vya kutosha. Nataka wana Iringa waingie kwenye sekta hii na tufanye wenyewe.”

Alitaja maeneo kama Ihomasa, Ihanzutwa, Sinai, Ulata, Igomaa, Mlima Kitonga, Image, Kiwele na Mtera kuwa na fursa kubwa za madini, akisema yataleta fursa za ajira na mapato kwa vijana.

“Najiandaa kuwatengeneza wana Iringa kuingia sekta ya madini. Tutawafundisha, tuwasaidie kupata leseni ndogo, tuwe na migodi ya kwetu. Sitaki Iringa iwe ya mwisho, nataka tuwe wa kwanza kunufaika na ardhi yetu,” alisema kwa msisitizo.

Ngajilo aliongeza kuwa mbali na madini, miradi mingine mikubwa itatekelezwa ili kuinua uchumi wa Iringa, ikiwemo ujenzi wa stendi ndogo ya magari ya Dodoma, na mradi wa utalii wa Kihesa–Kilolo unaolenga kuimarisha utalii wa Kusini.

“Mradi wa utalii Kihesa–Kilolo sasa ni wakati muafaka. Tutakuwa na miradi kadhaa itakayosukuma utalii wa kusini, ikiwemo uwekezaji wa hoteli, bustani na vivutio vipya,” alisema.

Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Kihesa, Ngajilo alisema pia atashirikiana na halmashauri kuboresha miundombinu ya masoko, kuweka taa za barabarani na kusaidia wajasiriamali wadogo kupata mikopo yenye riba nafuu kupitia halmashauri, SACCOS na vikundi vya maendeleo.

Aidha, aliahidi kufufua timu ya Kihesa Stars, akisema michezo ni sehemu muhimu ya kuunganisha vijana na kujenga afya ya jamii.

“Kihesa Stars lazima irudi. Tunahitaji michezo iwe chanzo cha umoja na maendeleo katika kata hii,” alisema.

“Tunapozungumzia kuunda jiji, Kihesa ni sehemu ya mipango hiyo. Lazima tuipe kasi kubwa, tuipeleke mbele kwa nguvu za vijana na ubunifu,” alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, alisema yuko tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, hata kama ni kushiriki kwa kuchimba mitaro kwa maendeleo ya wananchi.

“Siasa ni mipango, lakini utekelezaji ni vitendo. Nipo tayari kushiriki bega kwa bega na wananchi kutekeleza Ilani ya CCM,” alisema.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button