Makonda aahidi neema kwa vijana

ARUSHA: MGOMBEA ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema wananchi wakimchagua atahakikisha vijana wanapatiwa mikopo na fursa mbalimbali.
Aidha, lengo ni vijana hao kujikwamua kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuachana na matukio ya uhalifu.
Makonda alisema hayo Oktoba 26 alipokuwa akipita mtaa kwa mtaa kuhamasisha wananchi kupiga kura Oktoba 29,mwaka huu.
Alisema anatambua kuwa wapo baadhi ya vijana wanaofanya matukio ya uharifu kwa sababu ya ugumu wa maisha, hivyo katika uongozi wake atawawezesha vijana kiuchumi vijana ili wafanye majukumu vizuri kwa kuibua fursa za kiuchumi ili kila vijana wawe na shughuli za kufanya.
“Usalama wa nchi ni jukumu la wananchi wote kuhakikisha maeneo wanayoishi yanakuwa salama,watoto wanafanya matukio ni watoto wetu kila mmoja anatakiwa kuwa sehemu ya ulinzi wa watoto kuanzia ngazi za familia,”alisema Makonda.
Aliahidi kuongeza thamani ya mabalozi na ngazi za mashina inarejeshwa, ili wawe walinzi wa ulinzi na usalama katika maeneo yao chini ya usimamizi wa wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ili kila kaya iwe salama.
“Ndani ya halmashauri kuna aina nne za mikopo inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani inayotolewa kwa wanawake, vijana na makundi kupitia ofisi mbalimbali za serikali kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawezeshaji kiuchumi vijana kiuchumi nao waondokane na ukosefu wa ajira na wananchi wanaelewa taratibu za mikopo hiyo na kuipata kwa urahisi,”alisema.
Makonda alisema Tanzania bado haijafikia kiwango cha uzalishaji wa kutosha kwa sababu gesi nyingi zinaagizwa kutoka nje ya nchi, huku matumizi yake yakiongezeka zaidi ya uzalishaji wa ndani.
Alisema jimbo hilo bado lipo nyuma katika miundombinu ya barabara, hivyo atahakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Aidha,aliwaomba wananchi kujitokeza kupiga kura ili wasipoteze haki yao ya msingi kwa sababu maamuzi watakayoyafanya ndio yataamua uelekeo wa taifa katika kipindi cha miaka mitano.



