Amani yatawala Mtwara uchaguzi mkuu

MTWARA: MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewakikishia hali ya amani na usalama wananchi mkoani humo wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Oktoba 27,2025 mkoani Mtwara, mkuu huyo wa mkoa amesema viongozi wao hao wamejipanga vema kuhakikisha hali ya amani na usalama inatawala kwenye mkoa huo.
“Ndugu wananchi sisi viongozi wenu wa mkoa tumejipanga vema kuhakikisha hali ya amani na usalama inatawala siku ya kupiga kura na niwahakikishie kuwa mkoa wetu hali ya usalama ni shwari,”amesisitiza Sawala.

Ameongeza kuwa: “Niwasihi nyote wenye sifa za kupiga kura mjitokeze kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu kwani vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo kazini”.
Aidha, amewasihi wananchi hao baada ya kukamilisha zoezi hilo la kupiga kura wahakikishe wanaondoka eneo hilo la tukio ili wakaendelee na majukumu yao mengine ili kuepuka uvunjifu wa kisheria.
Ameendelea kuwasisitiza wananchi hao kuwa ushiriki wao katika kupiga kura utawapa fursa ya kikatiba ya kuchagua viongozi bora watakaoshirikiana nao kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.



