Mamia wajitokeza kwa matibabu bobezi

MAMIA ya wakazi wa Dodoma wameitikia wito wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dk Frederick Sagamiko kufika kwenye matibabu bila malipo yanayotolewa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na watalaamu wa afya bobezi na mabingwa bobezi waliosoma Korea Kaskazini.
Akizungumza Ofisa Utumishi Mkuu katika Wizara ya Afya, Athuman Masesa alisema matibabu hayo yanatolewa kwa watu wote bure na watakaobainika kuwa na changamoto za afya zao watapewa rufaa katika kituo cha Afya cha Makole. “Wagonjwa watakaobainika kuwa na changamoto, watapewa rufaa kwenda kuendelea na matibabu katika Kituo cha Afya cha Makole jijini Dodoma,” alisema Masesa.
Amesema kliniki hiyo imekuwa ikifanyika kila mwaka, kwa ushirikiano na taasisi hizo, ambazo ni kutokana na makubaliano baina ya Wizara ya Afya ya Tanzania na Korea Kaskazini wasomi wanaotoka nchini huko kutumia taaluma zao kusaidia wananchi kupata huduma hizo.SOMA: NIMR yaja na utafiti wenye virusi vya Ukimwi, kisukari
Amesema wataalamu bingwa na bingwa bobezi wanatumia utaalamu waliopata wakiwa kwenye mafunzo Korea Kaskazini kusaidia wagonjwa kwenye magonjwa yasiyoambukiza kuwachunguza na kuwapa msaada wa awali. Magonjwa yatakayopimwa ni kisukari, saratani ya matiti, shinikizo la juu la damu, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya kibofu cha mkojo. Wagonjwa wengi waliojitokeza ni wanawake, hivyo Masesa ameshauri vijana pia wajitokeze kupima na kufanya uchunguzi wa afya zao, kwani kwa sasa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanasababisha vifo vingi.



