Afrika yashauriwa kuboresha afya kwa akili mnemba

ARUSHA: SERIKALI za Afrika ikiwemo Tanzania, hospitali binafsi na wataalamu wa teknolojia wamehimizwa kushirikiana katika kuunda mikakati ya kitaifa ya huduma za afya zinazotumia akili mnemba, ili kuongeza ufanisi na ubunifu katika sekta hiyo.

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkutano wa Kilele wa Akili Unde Afrika (APAIC 2025), Abdulwahid Ali Khamis, amesema sekta ya afya barani Afrika kwa muda mrefu imekabiliwa na changamoto za uhaba wa fedha, rasilimali watu na miundombinu, lakini sasa mabadiliko chanya yanaanza kuonekana kupitia matumizi ya teknolojia za akili bandia.

“Teknolojia ya kizazi kipya ya akili unde, inayoitwa Agentic AI, imepiga hatua kubwa. Sasa siyo tu kuchambua taarifa, bali inaweza kufanya maamuzi, kuchukua hatua na kushirikiana na binadamu kwa wakati halisi. Badala ya kuchukua nafasi ya binadamu, teknolojia hii inakuwa mshirika wa madaktari, wasimamizi wa hospitali na maafisa wa afya,” amesema Khamis.

Ameeleza kuwa wingi wa vijana barani Afrika, ukuaji wa miundombinu ya kidijitali na ongezeko la wataalamu wa teknolojia ni fursa kubwa ya kuifanya Afrika kuwa kinara katika huduma za afya za kidijitali.

Kwa sasa, wabunifu wengi barani humo wanaunda hospitali za kisasa zilizounganishwa na mifumo ya akili bandia, maabara zenye uwezo wa kidijitali, na programu za afya za jamii zinazohusishwa moja kwa moja na mtandao.

Khamis ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za elimu na wadau wa maendeleo kushiriki mkutano wa APAIC 2025 utakaofanyika jijini Arusha, ambapo kutasainiwa. Tamko maalumu la Kimataifa kuhusu matumizi salama na yenye maadili ya akili bandia katika huduma za afya.

Amesema mafanikio ya teknolojia hiyo yanategemea uwekezaji katika miundombinu ya taarifa, viwango vya maadili na mafunzo ya kidijitali kwa wataalamu wa afya.

“Kwa kutumia akili bandia katika kazi za kawaida, madaktari wanapata muda zaidi wa kuwahudumia wagonjwa. Katika dharura, mifumo hiyo inaweza kubadilisha taarifa kuwa hatua za haraka, jambo linaloweza kuokoa maisha,” ameongeza.

Kwa sasa, baadhi ya hospitali barani Afrika zimeanza kutumia mifumo hiyo kusaidia kupanga vipaumbele vya wagonjwa, kutabiri milipuko ya magonjwa na kurahisisha utambuzi wa maradhi kwa haraka.

Wataalamu wanasema kuwa endapo mwelekeo huo utaendelezwa, Afrika inaweza kuwa mfano wa dunia katika utoaji wa huduma za afya za kisasa, jumuishi na zenye kumweka binadamu mbele ya teknolojia.

Aidha, wamependekeza utekelezaji wa mwongozo wa bara wa kukuza uelewa wa akili Unde, pamoja na kuongeza uwekezaji katika kampuni changa za teknolojia na miundombinu yake, ili kuimarisha uhuru wa kiteknolojia na kuchochea ubunifu endelevu.

Khamis amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili katika matumizi ya teknolojia hizo, akibainisha kuwa viongozi wa teknolojia barani Afrika wanaendelea kuweka kanuni za kulinda faragha za wagonjwa, usalama wa taarifa na upatikanaji sawa wa huduma.

Mkutano wa APAIC 2025, unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha, utakuwa jukwaa kubwa la kujadili maendeleo ya akili bandia na mageuzi ya kidijitali katika sekta ya afya barani Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button