Wakili msomi Chaula ausaka umeya Iringa Mjiini
IRINGA: Wakili msomi, Jackson Chaula, Diwani wa Kata ya Mlandege, amejiweka rasmi kwenye ramani ya kinyang’anyiro cha Umeya wa Manispaa ya Iringa baada ya kurejesha fomu yake leo, Novemba 21, 2025, hatua inayomweka katika duru ya mwisho ya mchujo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chaula sasa anasubiri maamuzi ya chama yanayotarajiwa kuvuta hisia za kisiasa ndani ya CCM Iringa Mjini ili kutoa jina litakalosimama kuongoza Manispaa ya Iringa kwa miaka mitano ijayo.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM Iringa Mjini, Wakili Chaula alitoa dira ya uongozi anaoutizamia kuupeleka kwenye meza ya madiwani, akisema Iringa iko katika kipindi kinachohitaji uongozi mahiri, shirikishi na wenye uelewa mpana wa mifumo ya kisheria na kiutawala.
“Uongozi ni fikra, maoni, ubunifu na uwezo,” alisema kwa msisitizo.
“Iringa inahitaji kiongozi atakayekusanya nguvu za watu wote. Wananchi ndio wamiliki halisi wa serikali yao, na mimi nitaweka uzito mkubwa kwenye ushirikishwaji wao.”

Amesema endapo atapata ridhaa ya chama na hatimaye ya Baraza la Madiwani, ataendesha halmashauri kwa kuzingatia misingi ya uwazi, nidhamu ya matumizi ya fedha na utekelezaji wa miradi kwa mujibu wa sheria — misingi anayoiita “nguzo za halmashauri yenye tija na ufanisi.”
Katika kauli iliyobeba uzito wa kisiasa, Chaula alisema kiongozi wa sasa anapaswa kuwa daraja la maridhiano, si kiini cha mgawanyiko.
“Kazi ya kiongozi ni kuunganisha watu. Mimi nitaunganisha wananchi, madiwani na watendaji wa halmashauri ili kuisogeza Iringa mbele na kuifungua kiuchumi zaidi kuliko ilipo leo,” alisema.
Kwa upande wa uwezo na uzoefu, Chaula alisema amejipima vya kutosha kama mwana-CCM na kama mtaalamu wa sheria, na kuona anayo nafasi ya kuisukuma Manispaa kutoka hatua moja ya maendeleo kwenda nyingine.
Kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM kinatarajiwa kuwa na ushindani mkali, kwani wengine waliorejesha fomu ni Meya aliyemaliza muda wake, Diwani wa Mshindo Ibrahim Ngwada, na Diwani wa Mkimbizi Elliud Mvella.



