Mashauri Mwenyekiti mpya Halmashauri Kwimba

MWANZA; MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya Kwimba mkoani Mwanza wamemchagua Lameck Mashauri wa Cbama Cha Mapinduzi(CCM) kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kupata kura za ndiyo 42 kati ya kura 43 zilizopigwa, ambapo kura moja iliharibika.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Gervas Kitwala alishinda kwa kura 41 za ndio huku kura 2 ziliharibika. Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Halmshauri ya Kwimba.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mashauri alishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumteua kuwa mgombea pamoja na madiwani wote kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuongoza.

“Nawashukuru sana kwa kuniamini. Miaka mitano iliyopita nilitumika kama Makamu Mwenyekiti imenipa uzoefu wa kusimamia na kutekeleza miradi. Naomba muendelee kuniunga mkono ili tuifikishe mbali Halmashauri yetu ya Kwimba ,”alisema.

Aliahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano na madiwani wote ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi inatekelezwa kikamilifu.

“Tushikamane kwa pamoja ili kutimiza tuliyowaahidi wananchi. Dhumuni ni kuona Kwimba ikipiga hatua kubwa kufikia maendeleo tunayotamani hadi mwaka 2030,” amesisitiza.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti mpya aliyechaguliwa Kitwala alisema yuko tayari kushirikiana na uongozi, madiwani na watendaji kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Mbunge wa Jimbo la Kwimba, Cosmas Bulala amewataka viongozi wa halmashauri, madiwani na wananchi kuendelea kushikamana kusimamia, kushauri na kutekeleza maamuzi yanayolenga kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika kikao cha halmashauri, Mbunge Bulala alisema hatua ya wananchi kuchagua viongozi wao ni jambo kubwa na la kupongezwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anashiriki kikamilifu kuongeza tija ya utendaji kazi wa halmashauri.

“Tumefanya uamuzi mzuri kuchagua viongozi wetu, tuisimamie halmashauri yetu na tuishauri vyema, ili tufikie malengo. Tumeahidi mambo mengi hivyo ni lazima tuyatekeleze kwa vitendo,” alisema.

Katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Sumve, Moses Bujaga amewataka viongozi na watendaji kufanya kazi bila upendeleo, kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.

“Tufanye kazi bila upendeleo. Madiwani tuoneshe ushirikiano na wananchi nao wawe sahihi katika kushirikiana na watu wanaowahudumia,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button