Jamii yakumbushwa kuzingatia lishe bora

ARUSHA; JAMII imekumbushwa lishe bora ni msingi wa afya ya binadamu, lakini pia izingatie usafi ili kujikinga magonjwa ya milipuko.
Hayo yamesemwa na Ofisa Tawala Wilaya ya Monduli, Anael Mbise kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, Gloriana Kimath katika maadhimisho ya wiki ya lishe kitaifa, ambapo kiwilaya yalifanyika Kata ya Meserani eneo la Dukabovu.
Pia amesesisitiza jamii kufanya mazoezi zaidi na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta vinavyoweza kuleta madhara.

Naye Dk George Kasibante ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, amesema afya bora ni pamoja na kujikinga na magonjwa ya mlipuko, hivyo jamii pia izingatie usafi wakati wote ikiwemo kunawa maji kwa sabuni.
Akizungumza wakati wa utoaji elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe bora , Adventina Nyambuya amewaasa wananchi wa Monduli namna nzuri ya ulaji wa nyama pamoja na kupunguza matumizi ya sukari.



