Matumizi ya dawa za kienyeji yaongeza wagonjwa wa figo

KILA mwaka inapofika Novemba 15, 2025 Tanzania hufanya maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukizwa, magonjwa ambayo kwa sasa yanatajwa kuwa chanzo kikubwa cha vifo vya wagonjwa wengi. Tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa zinaonesha kuwa magonjwa hayo yanasababisha vifo vya watu wengi kwa asilimia zaidi ya 70.

Magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la damu, figo, kisukari, saratani na magonjwa ya mifumo ya mwili ambapo kati ya hayo, magonjwa ya kisukari pamoja na moyo ndiyo yanaongoza kwa kusababisha vifo. Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kuongezeka kwa wingi kwa wagonjwa wenye magonjwa hayo inasababishwa na mtindo mbaya wa maisha, ikiwemo ulaji wa vyakula usiofaa katika familia nyingi.

Wataalamu hao wanaeleza kuwa matumizi ya vyakula vyenye wanga mwingi huzalisha sukari ambayo ndiyo imekuwa kisababishi kikubwa cha magonjwa hayo, huku suala la mazoezi likisaulika kwenye jamii. Wakati suala la ulaji wa vyakula visivyofaa likitajwa kuwa chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa wagonjwa wenye magonjwa hayo, matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kienyeji nayo yanatajwa kuwa chanzo pia.

Kama ilivyo utamaduni wa jamii nyingi hapa nchini, matumizi ya dawa za kienyeji yamekuwa jambo la kawaida katika kujitibu magonjwa mbalimbali. Wataalamu wa afya wanasema licha ya matumizi ya dawa hizo kukubalika kitaalamu lakini changamoto ambayo imeanza kujitokeza ni matumizi yaliyopitiliza ya dawa hizo.

Katika Mkoa wa Simiyu wakati wa kuadhimisha wiki ya magonjwa hayo, Mratibu wa Huduma za Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Dk Juma Muna anasema matumizi yaliyopitiliza ya dawa hizo imekuwa chanzo cha kuongezeka wagonjwa wa figo.

Dk Muna anasema wananchi wengi wa Mkoa wa Simiyu wamekuwa na utamaduni wa kujitibu magonjwa kwa dawa za kienyeji wakiwa majumbani mwao. Anaeleza wakati wanajitibu magonjwa hayo kwa dawa za kienyeji, dawa hizo zinapoingia mwilini kutokana na kutumika bila utaalamu, basi moja kwa moja zinakwenda kuharibu figo na ini.

Dk Muna anasema wananchi wanapotumia dawa hizo wanaona ni jambo la kawaida lakini kutokana na kutumia bila vipimo, basi zimekuwa zikiharibu mfumo mzima wa figo. Anabainisha katika kipindi cha hivi karibuni katika mkoa huo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo ambao wamekuwa wakipokelewa katika hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa.

Anasema asilimia 90 ya watu ambao wamekuwa wakija, wamekutwa katika hali mbaya ya figo kutofanya kazi ambapo chanzo kikubwa wamegundua ni kutumia kwa kiwango kikubwa dawa za kienyeji. Dk Muna anaeleza elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa hizo ndiyo mwarobaini

Kwa kupambana na changamoto hiyo mpya kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala ndiyo wenye jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya dawa hizi za kienyeji. Licha ya kusimamia, wanao wajibu wa kutoa elimu kwa jamii katika kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa hizo.

Licha ya uwepo wa mamlaka hiyo, wataalamu wa afya katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya kama zahanati na vituo vya afya, hasa maeneo ya vijijini hawana budi kubeba jukumu hili. Kama wataalamu wa afya wenyewe wanathibitisha kuwa tatizo linazidi kuongezeka, ni wakati sasa wa elimu kutolewa kwa nguvu kubwa kunusuru maisha ya wananchi na matumizi ya dawa hizi.

Elimu ndiyo itakuwa mwarobaini wa kupambana na changamoto hii mpya katika jamii yetu. Wananchi wanatakiwa kupata elimu na kuelezwa matumizi sahihi ya dawa za kienyeji. SOMA : Ugonjwa wa figo wa nane kuua duniani

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button