Ugonjwa wa figo wa nane kuua duniani

DAR ES SALAAM: Watu milioni 850 duniani wanasumbuliwa na magonjwa sugu ya figo na kati yao watu milioni 3.1 hufariki dunia kila mwaka na kuufanya ugonjwa huo kushika nafasi ya nane ulimwenguni kwa kusababisha vifo.
Hayo yamesemwa leo Machi 14,2024  na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dk Jonathan Mngumi wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza figo dhidi ya magonjwa ikiwa ni siku ya maadhimisho ya figo duniani ambayo huadhimishwa mwezi Machi kila mwaka.
Mngumi amesema watu wengi wenye magonjwa ya figo wanakadiriwa kuishi katika nchi zinazoendelea hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na kwa sasa inakadiriwa kuwa wastani wa asilimia saba mpaka 25 ya wakazi wa Afrika wana matatizo ya figo ambapo kiasi hiki ni mara tatu zaidi ya nchi zilizoendelea, ” amesema Dk Mngumi na kuongeza
“Idadi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma ya kusafisha damu imefikia 3,500 nchini kote ambapo kwa Muhimbili kila siku inahudumia wagonjwa 120 hadi 130,” amesema.
Aidha,  Mngumi ameitaka jamii kubadili mtindo wa maisha kuacha matumizi makubwa ya sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na shinikizo la damu ambayo yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya figo.
Kauli mbiu mwaka ya huu inasema “Afya ya figo kwa wote, kuendeleza usawa katika ufikiaji wa huduma na matumizi bora ya dawa”