Ulega: Vijana lindeni amani

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa wito kwa vijana walinde amani ya Tanzania. Ulega alisema amani ni nguzo ya maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi. Amesema hayo wakati akikagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa Barabara ya Mabatini na Daraja la Mkuyuni jijini Mwanza jana akitekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliyoyatoa hivi karibuni mkoani humo.
Ulega amesema uwepo wa amani unaiwezesha serikali kutekeleza miradi ya kimkakati bila usumbufu.Katika eneo la mradi wa upanuzi wa Daraja la Mabatini na barabara unganishi yenye urefu wa meta 590, Ulega alimpongeza mkandarasi kwa kazi anayofanya. “Wananchi wameridhika. Msongamano wa magari nao umepungua kwa kiwango fulani,” alisema Ulega na kuongeza kuwa upanuzi wa barabara mbili kwenda na kurudi umeongeza ufanisi wa usafiri katika eneo hilo.
Aidha, Ulega amewapongeza wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi kwa ubora na akasema serikali itaendelea kuwaamini na kuwapa kazi kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kuongeza ajira kwa Watanzania. “Fedha inayolipwa kwa mkandarasi mzawa inabaki hapa nchini na kuchochea uchumi wetu, hivyo fanyeni kazi nzuri,” alisema.
Ulega amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose ahakikishe kuna ufumbuzi wa kudumu wa msongamano wa magari jijini Mwanza. Pia, ameagiza ziwekwe taa za barabarani katika maeneo ya Mabatini na Mkuyuni ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi nyakati za usiku. Kwa upande wake, Ambrose alisema ujenzi wa Daraja la Mabatini na barabara yake unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na sasa umefikia asilimia 93.
Amesema lengo kuu la ujenzi wa daraja hilo na barabara unganishi ni kutatua changamoto za mafuriko yaliyokuwa yanatokea mara kwa mara, kutokana na mvua za El Niño kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024. Kwa mujibu wa Ambrose mradi huo unatekelezwa kwa thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.3 na unahusisha ujenzi wa boksi kalvati lenye milango sita ya kupitisha maji, kila mmoja ukiwa na upimaji wa meta nne kwa meta mbili na nusu.
Ambrose amesema upana wa daraja umeongezeka kutoka meta 15 hadi 26.1 na barabara ikijengwa kwa upana wa meta 30 na njia nne. Amesema mradi huo ulianza Novemba 15, mwaka jana na ulitarajiwa kukamilika Novemba 11, 2025 lakini kutokana na changamoto za kuhamisha miundombinu ya maji na umeme, mkandarasi aliongezewa siku 45 na sasa unatarajiwa kukamilika Desemba 30, mwaka huu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa Daraja la Mkuyuni na barabara unganishi ya meta 500, Ambrose alisema mradi huo pia unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 5.1 na umefikia asilimia 7. SOMA: Watanzania tusimamie misingi, utu wema kulinda amani ya nchi



