FCC yapewa maagizo 5 vita dhidi ya bidhaa bandia

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeitaka Tume ya Ushindani (FCC) kuimarisha na kupanua matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi, ufutiliaji wa udhibiti wa bidhaa bandia katika masoko ya kidijitali.

Pia FCC imetakiwa kuongeza kasi ya uratibu na ushirikiano wa karibu na taasisi zingine za udhibiti, ikiwemo vyombo ya dola na mamlaka za forodha ili kuhakikisha taarifa zinashirikishwa kwa wakati na hatua zinachukuliwa haraka dhidi ya bidhaa bandia.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia 2026 yaliyofanyika leo Juni 25, Dar es Salaam.
Katika maadhimisho hayo, Mapunda ametoa maagizo matano, ikiwemo FCC kuimarisha elimu kwa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia, ikiwemo kampeni za kitaifa zinazolenga kuwafikia watumiaji wa mwisho wa bidhaa wakiwemo wafanyabiashara na makundi maalumu.

Aidha, ameitaka FCC kuendelea kujenga ushirikiano wa moja kwa moja na wamiliki wa alama za biashara na sekta binafsi ili kuboresha mifumo ya utambuzi wa bidhaa bandia na kurahisisha utoaji wa taarifa na ushahidi wa kitaalamu wakati wa uchunguzi.

“Tume iendelee kuimarisha uwezo wa rasilimali watu, kupitia mafunzo ya mara kwa mara, ili kuongeza ufanisi katika uchunguzi, uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa sheria dhidi ya wahusika wa biashara za bidhaa bandia,” amesema Mapunda katika agizo lake namba tano.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti, Kamishna wa FCC, Said Tunda amesema tume hiyo imeendelea kuimarisha mifumo ya kuhakikisha wanapambana katika kudhibiti bidhaa bandia. Pia tume hiyo inatarajia kuongeza uwezo wa kuondoa bidhaa bandia kwa wakati.

“Pia tume inatarajia kuongeza ushirikiano na wamiliki wa alama za bidhaa, kuongeza elimu kwa umma pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za ukaguzi na ukaguzi,” amesema Tunda.



