Tandahimba yapata hati safi

MTWARA: HALMASHAURI ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara imepata hati safi ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Yamejiri hayo wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Tandhahimba kuhusu kujadili hoja za hesabu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAC) pamoja na maagizo ya Kamati ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.

Akiwasilisha taarifa hiyo ya CAG mbele ya baraza hilo, Mkaguzi Mkuu wa Nje, Andindilile Mwabwangwa amesema ripoti ya CAG mwaka 2024/2025 iliwasilishwa kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo ikiwa na mapendekezo ishirini na tisa.
‘’Ofisi yangu ilipokea taarifa ya utekelezaji na kwa kushirikiana na wataalam wa halmashauri ya wilaya ya tandahimba tulifanya uhakiki ambapo mapendekezo ishirini na tano yalifanyiwa kazi kikamilifu sawa na asilimia 86 na hivyo mapendekezo manne yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,’’amesema Mwabwangwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi ameipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi na kwamba mafanikio hayo ni matokeo ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, uwajibikaji wa viongozi pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora.
Pia amewataka viongozi wa halmashauri kuendelea kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maenedeleo inayotelekelezwa kwenye halmashauri hiyo ikiwemo ya sekta ya elimu, maji, afya na mingine.

Mbali na hilo amesisitiza suala la kuendelea kusimamia marejesho ya mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na halmashauri kupitia mapato yake ya ndani inayotolewa kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ikiwemo vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.



