RC Kheri: Haki ni chanzo cha amani na maendeleo

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema umoja na mshikamano wa Watanzania, amani ya nchi na maendeleo yanayoonekana leo ni matunda ya haki.

RC Kheri aliyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama hiyo, chini ya kauli mbiu “Safari ya Miaka 20: Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda.”

Amesema Mahakama ni muhimili uliopewa dhamana ya kutafsiri sheria, hivyo ni wajibu wa taasisi zote na wananchi kwa ujumla kuilinda, kuiheshimu na kushirikiana nayo ili haki itolewe kwa wakati.

“Amani yetu ni tunda la haki, na maendeleo yetu ni matokeo ya haki. Mahakama hii lazima iendelee kutoa haki kwa weledi, uadilifu na bila upendeleo,” alisema RC Kheri.

Amepongeza ushirikiano uliopo kati ya mawakili wa Serikali na wale wa kujitegemea, akisema ni kielelezo kizuri katika utetezi wa mashauri na uimarishaji wa mfumo wa haki.

RC Kheri pia alisisitiza umuhimu wa taasisi za haki kama Polisi, Magereza na TAKUKURU kushirikiana kwa karibu na Mahakama, hususan katika kuhakikisha ushahidi unapatikana kwa wakati ili mashauri yasikwame.

Katika hatua ya vitendo, Serikali ya Mkoa imesema itabeba jukumu la kujenga eneo la kivuli kwa ajili ya wananchi wanaofika mahakamani, ili kujikinga na jua na mvua.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dunstan Ndunguru, amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, mahakama hiyo imepiga hatua kubwa katika utoaji wa haki.

Amesema maboresho makubwa yamefanyika katika matumizi ya TEHAMA, ambapo mashauri sasa yanasajiliwa na kusikilizwa kwa njia ya mtandao, hatua iliyopunguza ucheleweshaji wa haki.

Jaji Ndunguru amesema miundombinu iliyopo, licha ya kutokujengwa awali kwa matumizi ya Mahakama, imefanyiwa usanifu na maboresho hadi kukidhi viwango vinavyohitajika na kuwezesha shughuli za Mahakama kufanyika kwa ufanisi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa Moses Ambindwile ameipongeza Mahakama kwa kutunza miundombinu yake, na kushauri kuongezwa kwa miundombinu kutokana na ongezeko la watumishi na wadau, ikiwemo maeneo ya kusubiria wasikilizaji wa kesi pamoja na vyoo vya kutosha kwa watumishi na wananchi.

Alitaja Mahakama Kuu Iringa kama zaidi ya chuo cha uongozi, akileza kuwa imetoa viongozi wengi wakubwa wa Mahakama na Serikali.

Akimwakilisha Jaji Kiongozi katika maadhimisho hayo, Jaji Imani Aboud aliwakumbusha Majaji na Mahakimu kuwa Mahakama inatenda haki kwa niaba ya Mungu, hivyo ni wajibu wao kuitenda haki hiyo kwa kuzingatia utu, usawa na heshima kwa kila mwananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button