Walanguzi tiketi za abiria kikaangoni

GEITA: JESHI la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani limekemea vikali tabia ya mawakala wa mabasi ya abiria kufanya ulanguzi wa tiketi wa safari za mwisho wa mwaka kwani watachukuliwa hatua.

Ofisa Mnadhimu Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Butusyo Mwambelo ametoa kalipio hilo baada ya zoezi la ukaguzi wa vyombo vya usafiri kituo cha mabasi mjini Geita.

SACP Mwambelo amesema mbali na mahitaji makubwa ya usafiri kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka maofisa usafirishaji wanapaswa kusimamia miongozo yote ya gharama na sheria za usafirishaji.

“Wajibu wa kondakita ni kuhakikisha watu hawaondoki stendi, kuhakikisha kila mtu ana tiketi, inayoendana na fedha aliyotoa pamoja na nauli inayoendana na maelekezo ya LATRA.

“Mawakala mmezidi, mwisho wa mwaka tufanye kazi tukiwa na hofu ya Mungu, kwa sababu mawakala mnachukua tiketi zote za mtandaoni gari zima au nusu ya gari”, amesema Mwambelo.

Amesema wamebaini kuwa baadhi ya mawakala na makondakta wa mabasi ya mikoani wanalangua tiketi na kuziuza kwa bei ya juu hali inayoashiria utapeli kwa abiria.

“Mtu anaenda kutafuta tiketi ya safari, anaambiwa gari limejaa, au anaambiwa kuna siti moja imebaki, kwa sababu anashida anachukua hiyo tiketi kwa gharama ya juu” amefafanua SACP Mwambelo.

Aidha ametaja changamoto nyingine ya tiketi zilizolanguliwa ni kukosa taarifa sahihi za abiria na hivo pindi inapotokea ajali mara nyingi tiketi hizo zinakuwa majina tofauti na majina halisi ya abiria.

Ameagiza viongozi wa mawakala wa vituo vya mabasi nchini kuhakikisha wanakomesha tabia ya ulevi kwa mawakala wa mabasi kwani ndio chanzo cha utapeli na wizi.

Kaimu Ofisa Usalama wa Barabarani mkoani Geita, Lazaro Masembo amesema ufuatiliaji unaendelea kuwadhibiti makondakta na madereva wote wanaojihusisha kutapeli abiria ndani na nje ya vituo vya mabasi.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Aridhini (LATRA) mkoani Geita, Rajabu Selemani amesema milango ipo wazi kwa abiria wote kutoa taarifa kipindi wanapohisi kutapeliwa safarini.

Amesema LATRA inatekeleza wajibu wake na inafanyia kazi kwa wakati taarifa zote zinazotolewa na abiria ama wadau wa usafiri ili kukomesha tabia ya utapeli kwa maofisa usafirishaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button