Aagiza bajeti usafiri wa dharura kwa wajawazito
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba ameziagiza halmashauri za mkoa huo zijumuishe kwenye mipango na bajeti ya fedha gharama za usafiri wa dharura wa wanawake wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma za haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Mgumba alitoa agizo hilo Alhamis mjini Tanga wakati akizindua mpango wa dharura wa kuimarisha usafirishaji wa dharura kwa wanawake wajawazito wanaojifungua na watoto wachanga katika Mkoa wa Tanga.
Mpango huo umefadhiliwa na Vodacom Tanzania Foundation wakishirikiana na serikali, Touch Foundation na Pathyfinder International.
Lengo ni kuzuia vifo vya mama na mtoto kwa kuimarisha mfumo wa rufaa na usafiri wa dharura vijijini kupitia mfumo wa M- Mama.
Mgumba alisema wanawake wengi wajawazito wanapoteza maisha kwa sababu ya jamii kushindwa kufanya uamuzi wa haraka na muhimu kunapokuwa na dharura.
Alisema mpango huo umehakikisha huduma zinapatikana ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za dharura za upasuaji kutoka vituo 15 mwaka 2015 hadi vituo 27 mwaka 2022.
Mgumba alisema mkoa huo una magari 10 ya kubebea wagonjwa yanayofanya kazi ya kutolea huduma za dharura kwa wagonjwa kwenye vituo vya afya.
Awali Mkurugenzi wa M-Mama Tanzania kutoka Kampuni ya Vodacom Foundation, Dolorosa Duncan alisema mpango huo ni suluhisho la kiteknolojia katika kuimarisha rufaa na usafiri wa dharura kwa ajili ya wanawake wajawazito waliojifungua na watoto wachanga.
Alisema kupitia mpango huo, Vodacom inaunga mkono jitihada za serikali katika kuzuia vifo vya wanawake wajawazito na watoto kwa kuhakikisha wanaimarisha mfumo wa rufaa pamoja na usafiri wa dharura vijijini ili kuwaepusha na changamoto hizo.