Aagiza madeni ya wafanyakazi yalipwe kwa mapato ya ndani

MKUU wa Mkoa Arusha, John Mongella ametoa siku saba kwa halmashauri za Karatu, Longido na Arusha DC zilipe madeni ya wafanyakazi kwa mapato ya ndani.

Vilevile Mongella ameiagiza Halmashauri ya Ngorongoro iwalipe wafanyakazi bora wa mwaka jana zawadi zao hadi ifikapo Ijumaa wiki hii.

Alitoa maagizo hayo jijini Arusha jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani kimkoa.

Mongella alisema ni vizuri kila kiongozi akawajibika katika eneo lake kwa kuhakikisha anawasimamia wafanyakazi wake.

“Wafanyakazi wanafanya kazi zao vizuri, hivyo hakuna sababu ya viongozi kutowajibika kwao na fedha zinakusanywa, hakuna sababu ya kutowalipa wafanyakazi wao wanaotegemea stahiki zao kwa mapato haya, sasa natoa siku saba lipeni na nipate taarifa na nitafuatilia,” alisema na kuongeza:

“Mnapokusanya mapato haya kabla hayajaenda kwenye matumizi mengine, anzeni na wafanyakazi wenu waliofanikisha kupatikana kwa mapato haya.”

Kuhusu wafanyakazi bora kutajwa kwenye maadhimisho kisha waajiri wanawarusha au kuwapiga danadana wafanyakazi hao, alisema halikubaliki na hatapemda kulisikia likijirudia.

“Kwa kuwa Ngorongoro imelalamikiwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), nawaagiza hadi kufika Ijumaa wiki hii, muwe mmelipa stahiki zao wafanyakazi wenu bora wa mwaka jana na sio mkiwalipa hao iwe sababu ya kutolipa wengine wa mwaka huu hapana, mliwajua na kila mwaka mnajua kuna siku hii na hii kwa wote mnaowataja wafanyakazi bora kisha mnakaa kimya, sitataka kusikia hili, bora msiwataje, lakini mkiwasoma iambatane na stahiki zao.”

Alisema kwa sekta binafsi, nao ni lazima wafuate maagizo ya serikali ya ulipaji wa kima cha chini cha mishahara, kutekeleza hilo kwani kwa kutofanya hivyo ni kukiuka maagizo ya serikali.

Pia kwa kampuni zilizofungwa yakiwemo mashamba ya maua na kudaiwa na wafanyakazi wao, alishauri menejimenti zao zifuatwe kufahamu zaidi shida zinazowakwamisha kutekeleza hilo, japo baadhi anafahamu mchakato wa malipo unaendelea.

Mongella alikumbusha kwa waajiri hasa wa sekta binafsi wanaozuia kuanzishwa kwa matawi ya vyama vya wafanyakazi wahakikishe yanakuwepo, kwani sio takwa la mtu, bali ni sheria ya nchi na kwa kuzuia ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

Mwenyekiti wa Tucta Mkoa wa Arusha, Lotha Lazier alilalamikia Halmashauri ya Karatu, Arusha DC na Karatu, kuwacheleweshea stahiki zao wafanyakazi wao wanaolipwa kwa mapato ya ndani na kusababisha adha kubwa kwao, huku Halmashauri ya Ngorongoro ikiwapiga danadana wafanyakazi bora wa mwaka jana kuwalipa stahiki zao.

“Lakini tunasikitika sana kuona Halmashauri ya Ngorongoro mwaka jana siku kama leo, walitaja wafanyakazi wao bora, ila hawajawalipa hadi leo, tunafikisha kilio chetu serikalini, lakini serikali imetoa maagizo ya kima cha chini cha mshahara, ila baadhi ya sekta binafsi hawatekelezi maagizo haya ya serikali,” alisema.

Kuhusu kikokotoo alisema ni kaa la moto, sheria imetungwa na kupitishwa, lakini wanaomba ifanyiwe marekebisho ili kutoa ahueni kwa wafanyakazi.

Mratibu wa Tucta Mkoa wa Arusha, Daud Kamwela aliomba waajiri wanapotaja majina ya wafanyakazi bora kwenye maadhimisho hayo, iambatane na utoaji wa zawadi zao na sio kuwapiga kalenda kama ilivyofanyika kwa Halmashauri ya Ngorogoro mwaka jana.

Aliomba serikali kuhakikisha wastaafu wa sekta binafsi wanapata huduma ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kama ilivyo kwa wastaafu wa sekta ya umma kwa sababu wote wanachangia.

“Kitendo cha kuwanyang’anya wastaafu wa sekta binafsi vitambulisho vya bima ya afya, huku wakiachiwa wale wa sekta ya umma, ni ubaguzi tunaomba hili lifanyiwe kazi, kwani wote wamechangia wakiwa kazini,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button