CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kita wafuta uanachama wenyeviti wa mitaa na vijiji watakaokwenda kinyume na vipaumbele baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Novemba 27, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema hayo juzi akizindua kampeni za uchaguzi katika Kata ya Mpemba Jimbo la Tunduma mkoani Songwe.
Shaibu alisema chama hicho hakitamvumilia mwenyekiti yeyote atakayekandamiza wananchi kwa kwenda kinyume na vipaumbele walivyoainisha.
“Mnapochaguliwa mkatanguliza maslahi yenu ACT-Wa zalendo haitavumilia mwenyekiti yeyote wa mtaa anaye kwenda kinyume na vipaumbele nitavyosema hata kama ni kumfuta uanachama kwa sababu anakandamiza wananchi,” alisema.
Shaibu alisema wameahidi kupigania maslahi ya wafan yabiashara ndogondogo kwa sababu serikali za mitaa zina mchango katika mipango miji na kuwa wenyeviti wa mitaa wa chama hicho hawatakubali halmashauri wapange mipango ya kuwaondosha na kuwabughudhi wafanyabiashara ndogondogo.
Pia, alisema watawaagiza wenyeviti wake wakienda kwenye mabaraza ya kata wakasimamie huduma bora za kijamii kwa kutanguliza afya, maji na usambazaji wa uhakika wa umeme.
Tutawaagiza wenyeviti wetu wajue wao ni watumishi wa wananchi wasiende kuuza viwanja vya wazi wasimamie kulinda viwanja vya wazi, wasimamie haki kwenye masuala ya ardhi, wasimamie utoaji wa huduma nzuri katika ofisi za serikali za mitaa,” alifafanua Shaibu.
Chama hicho kimetaja vipaumbele 10 endapo itashinda nafasi za uongozi katika vijiji, mitaa ikiwemo kuhusisha wananchi kikamilifu katika uwekezaji wa ardhi.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa X kimeeleza kuwa kitahakikisha uwekezaji wowote unaohusu ardhi, wananchi wanahusishwa kikamilifu kama wabia.
Soma pia: Uchaguzi mitaa kutumia 4R za Rais za Samia
Kimetaja kipaumbele kingine ni kuzuia ardhi ya kijiji kumegwa ili kuwa hifadhi au kupewa mwekezaji bila ridhaa ya wanakijiji wenyewe. Vingine ni kuhakikisha miradi mipya yote ya majengo ya umma kama vile shule au hospitali inatumia nishati jadidifu kama vile umeme wa jua na kurudisha maeneo ya wazi yote mijini na kufuta tozo ya mauziano ya ardhi mijini.
ACT-Wazalendo pia ilisema itarudisha sauti ya wananchi kwa vijiji na mitaa yao kwa kuhakikisha kuwa mikutano mikuu ya vijiji na mikutano ya mitaa inafanyika kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.
Kingine ni kufuta malipo holela katika ofisi za serikali za mitaa na kuwa barua na mihuri itatolewa bila malipo.
Pia, kimeahidi kulinda raia dhidi ya ukamataji holela wa vyombo vya dola, kuwezesha wafanyabiashara wadogo ku fanya biashara bila bughudha kwenye mitaa ya miji, kuifanya mitaa kuwa misafi muda wote kwa kukusanya takataka kila wiki na kuanza kampeni mahususi ya kupanda miti ili kulinda mazingira