CHAMA cha ACT Wazalendo kimeridhia uamuzi wa Juma Duni Haji kujitoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa ACT Taifa.
ACT imefikia uamuzi huo baada ya kuketi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu iliyokutana kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema leo Machi 04, 2024.
Katika taarifa yake ya kujiondoa leo mchana huu imeeleza: “Nimekabidhi rasmi barua yangu kwa Katibu wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa na kuinakilisha barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Chama na Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchaguzi Taifa-kwa taarifa na hatua zao, kuhusu kuondoa nia (kujitoa) kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa.”
Juma Duni Haji alisema: “Nimechukua uamuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 11(3)(7) na Ibara ya 76(1)(p) na Ibara ya 111(3) zikisomwa pamoja, juu ya haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa Kiongozi, kazi na wajibu wa Halmashauri Kuu ya Chama kuwa ni “kujadili na kuidhinishwa majina ya wagombea wa nafasi za Kiongozi wa chama, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama”. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu kuridhia kujitoa kwangu katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo na kutopoteza muda wenu kutekeleza takwa la Katiba Ibara tajwa hapo juu”.