ACT yatoa wito kumaliza vurugu Msumbiji

CHAMA cha ACT- Wazalendo kimetoa wito kwa serikali kuhakikisha inadhibiti mpaka wa Msumbiji na mikoa jirani ya Tanzania ili kulinda usalama wa raia wake kufuatia kuibuka kwa vurugu nchini Msumbiji zilizosababishwa na matokeo ya uchaguzi.
Taarifa iliyotolewa leo Desemba 26, 2024 na Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nasra Nassor Omar imeeleza kukosekana kwa utulivu nchini humo kunaweza sababisha wimbi la wakimbizi na hatari za usalama kwa mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma.

“Tunaiomba SADC itoe kipaumbele cha utulivu wa Msumbiji kwa kufanya maamuzi ya kuingilia kati na kwa Umoja wa Afrika kusaidia masuluhisho endelevu. ACT Wazalendo tuwe tayari kusaidia juhudi hizi kusimamia haki na mshikamano pamoja na watu wa Msumbiji,” imeeleza taarifa hiyo.
Nasra Omar ameeleza katika taarifa hiyo kuwa Jukumu la Tanzania kama mwanachama mwanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Ulinzi ya SADC, Usalama kurahisisha mazungumzo kwa kuanzisha majadiliano kati ya wadau wote wa Msumbiji na kuhimiza chama cha Frelimo kufanya majadiliano kumaliza vurugu hizo.
Aidha, Mtandao wa New York Times wa nchini Marekani jana uliripoti kuwa watu 56 wamekufa tangu Jumatatu huku wengine wakijeruhiwa kufuatia vurugu za kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Msumbuji.

Kwa mujibu wa mtandao wa Al-Jazeera zaidi ya watu 30 wamekufa huku wafungwa 1,500 wakitoroka magerezani kufuatia vurugu hizo. Kwa mujibu wa kamanda wa polisi Bernardino Rafael ambapo aliongeza kuwa Jumatano wafungwa 150 waliokimbia gereza la Maputo walikamatwa tena.




