Adaiwa kuua mpenzi wake akimdai Sh. 100,000

MWANZA; POLISI mkoani Mwanza imemkamata mkazi wa Kijiji cha Kanyara wilayani Sengerema, Marwa Waryoba kwa tuhuma ya kumuua mpenzi wake.
Waryoba anatuhumiwa kumuua Nyabayango Nyahunge (45) mkazi wa Kijiji cha Kanyara, Kata ya Bulyaheke, halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Aprili 21, mwaka huu saa 2 usiku katika Kijiji cha Kanyara, Kata ya Bulyaheke.
Kamanda Mutafungwa alisema Bulyahela aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kuvuja damu nyingi na chanzo cha tukio hilo likielezwa ni wivu wa kimapenzi.
Alisema ilidaiwa Nyahunge na Waryoba Mwita walikuwa wapenzi na mtuhumiwa alimpa mpenzi wake Sh 100,000 za nyongeza ya mtaji wa kuuza pombe za kienyeji.
Mutafungwa alisema Aprili 19, mwaka huu mtuhumiwa alitaka alipwe fedha zake alizompa marehemu akidai kuwa anajihusisha kimapenzi na wanaume wengine, hali iliyozusha ugomvi baina yao na mtuhumiwa kufanya tukio hilo la kikatili la mauaji.
Wakati huohuo Polisi mkoani Mwanza wamemkamata mganga wa tiba asili na mmiliki wa nyumba ya kulala wageni ya Private Lodge, Edward Kumalija (38) ambaye pia ni mkazi wa Nyamhongolo, Manispaa ya Ilemela kwa tuhuma za kujipatia Sh milioni 12.5 kwa njia ya udanganyifu.
Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Aprili 18, mwaka huu saa 7 mchana katika Mtaa wa Shamaliwa, Kata ya Igoma wilayani Nyamagana.
Alisema mtuhumiwa huyo alijipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Edward Bihemo (43), ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyakabungo na mkazi wa Mtaa wa Nyamanoro, Kata ya Nyamanoro, Ilemela.
Alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa kumlaghai Bihemo kupitia kazi yake ya uganga wa tiba asilia kuwa ana uwezo wa kuzalisha fedha kwa njia ya miujiza. Chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kupata utajiri.
Alisema Kumalija alikuwa akichukua fedha hizo na kuziweka katika begi lake na kumuamuru Bihemo awe anazitolea sadaka mara kwa mara ili ziongezeke.
Mutafungwa alisema Bihemo aliendelea kutoa sadaka kwa muda mrefu hadi akakosa fedha ya kujikimu na akaamua kwenda kwa mtuhumiwa ili ampe fedha alizowekeza na ndipo alipogundua kuwa alikuwa ametapeliwa.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na Boniface Antony (33), mkulima na mkazi wa Mtaa wa Nyerere, Kata ya Igoma, Nyamagana ambaye pia ni mshiriki katika tukio hilo la kitapeli.