Afrika kusini kubadili sarafu zake kuruhusu lugha 11

BARAZA la Mawaziri la Afrika Kusini limeidhinisha muundo mpya wa sarafu ambao utakuwa na maandishi katika lugha 11 rasmi za taifa hilo tajiri namba tatu kwa uchumi Afrika.
Kila mwaka katika kipindi cha miaka 10 kutakuwa na sarafu yenye angalau lugha moja na kwa maana hiyo kutakuwa na mpishano kati ya lugha moja na nyingine.
Hii ni mara ya nne Afrika Kusini itakuwa inabadilisha muundo wa sarafu zake – ya mwisho ikiwa mwaka 1989.
Baraza la mawaziri katika taarifa iliyotolewa leo Sept. 2 lilieleza jinsi muundo mpya utakavyokuwa kwa kila Lugha.
“Neno “Afrika Kusini” litawekwa upande mmoja wa sarafu na kuchapishwa katika lugha zote rasmi. Lugha tatu zitatumika katika sarafu ya R5; lugha mbili sarafu ya R2; 50c, 20c na 10c na lugha moja itatumika kwenye sarafu ya R1,” taarifa ya baraza la mawaziri ilisema.
Sarafu mpya zitaanza kuzunguka mwaka ujao na bado hakuna muundo wa sampuli uliotolewa.
Afrika Kusini ina lugha 11 rasmi: Kizulu, isiXhosa, Kiafrikana, Sepedi, Setswana, Kiingereza, Sesotho, Xitsonga, Siswati, Tshivenda na Ndebele.