Afurahishwa na ukuaji wa sekta ya mawasiliano Z’bar

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Khalid Salum Mohamed amesema miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya mawasiliano hapa nchini.

Alisema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Tehama yaliyofanyika mjini Zanzibar.

“Nimearifiwa pia kuwa, hadi mwezi Machi 2023, idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka hadi kufikia watu milioni 33 na idadi ya watumiaji laini za simu kufika milioni 61.

Hii inaonesha kwamba Tanzania ni nchi ambayo watu wake wanaweza kupata huduma mbalimbali za mawasiliano kwa gharama nafuu ikilinganishwa na nchi nyingine duniani,” alisema.

Alisema mazingira ya uboreshaji wa mawasiliano yamesaidia utoaji wa huduma za kijamii, kufikia watu wengi zaidi katika maeneo ya mijini na vijijini, kuzalisha ajira, kuongeza pato la taifa, kufungua fursa mpya za maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini na hivyo kuboresha maisha ya wananchi.

Mohamed alisema serikali zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanapata ujuzi wa kutumia teknolojia za kidijitali kwa lengo la kuwaendeleza kiuchumi, kielimu na kijamii.

Aliwataka wakuu wa vyuo na shule za sekondari hapa Zanzibar kuhakikisha kuwa kila chuo na shule ya sekondari inakuwa na klabu ya kidijiti ili kuwahamasisha vijana kupata ujuzi wa Tehama ambao utasaidia kuleta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari alisema Siku ya Wasichana na Tehama Duniani, huadhimishwa kila mwaka na imetokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) na TCRA ni mwakilishi wa Tanzania katika shirika hilo.

Alisema kuwa TCRA kwa kushirikiana na wadau wa elimu yaani (TAMISEMI, Wizara ya Elimu, TCU na NACTVET) kwa sasa wanaandaa mwongozo utakaoelezea bayana namna ya kuanzisha na kuendeleza klabu za kidijiti katika shule za msingi, sekondari na vyuo.

Dk Bakari alisema wanathamini mchango wa sekta ya mawasiliano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuona wasichana katika Taifa hili wanapata fursa ya kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupata wataalamu watakaolisaidia Taifa kupiga hatua zaidi katika maendeleo hasa ukuzaji wa uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu.

Dk Bakari alisema kuwa kaulimbiu ya Siku ya Wasichana na Tehama duniani mwaka huu inasema “Ujuzi wa Kidigiti kwa Maisha” lengo la kaulimbiu hii ni kuhamasisha mafunzo na ujuzi wa kidijiti kwa wasichana na wanawake ili kuongeza ubunifu katika sekta ya Tehama kama tunavyofahamu kuwa msingi wa maendeleo katika jambo lolote ni kupata mafunzo sahihi na kutumia taaluma hiyo kwa manufaa yako binafsi na jamii kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button