Agizo la Rais Samia miche ya minazi latekelezwa

AGIZO la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kuwapatia miche ya nazi wakulima wa Mtwara na Lindi limetekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kwa kuwa ipo katika hatua ya uzalishaji.

Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano katika Kituo cha TARI Mikocheni, Vidah Mahava amesema hayo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Amesema pamoja na kutekeleza agizo hilo la Rais Samia, mahitaji ya miche kwa wakulima wengine ni makubwa kutokana na hamasa iliyofanywa na kituo hicho, hivyo ile inayozalishwa na TARI haitoshelezi.

Advertisement

“Kwa sasa hivi hata miche tunayoizalisha takribani 200,000 mingi itapelekwa Lindi na Mtwara ambako Rais Samia alitoa ahadi kwa wakulima kuwa atawapatia hiyo miche ya minazi,”amesema.

Amesema kwa kipindi hiki serikali imewapa fedha za maendeleo ambazo wamezitumia kwa ajili ya uzalishaji wa nazi.

“Ninavyozungumza kuna nazi nyingi ziko kwenye ardhi ambazo hazijaanza kuchipua na pale ambapo mdau atahitaji miche itabidi asubiri ifikie miezi sita mpaka nane,” amesema Mahava.