Apotheker yaiwezesha CDH kuboresha sekta ya afya kupitia Tehama
Asasi ya Apotheker ilianzishwa mnamo 2021 kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa jamii kupitia utafiti, mafunzo na ushauri.

DODOMA: Taasisi inayojihusisha na masuala ya afya nchini, Apotheker Health Access Initiative (AHAI), imekabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na samani za ofisi vyenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 27 kwa Kituo cha Afya Dijitali (CDH) kwa lengo la kusaidia juhudi za kuimarisha ujumuishaji wa suluhu za kidijitali katika sekta ya afya nchini.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta mpakato nne, projekta moja, kichapishi kimoja, meza mbili za ofisi, meza moja ya ofisi kwa watu wawili, viti kumi vya ofisi na makabati mawili ya kuhifadhia nyaraka.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika Jumatano, Juni 11, 2025, jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa TEHAMA wa wizara hiyo, Dk Silvanus Ilomo, aliishukuru AHAI kwa msaada huo unaolenga kuendeleza ajenda ya kidijitali katika sekta ya afya.
“Msaada huu utaimarisha kwa kiasi kikubwa juhudi za kituo katika matumizi ya TEHAMA kwenye huduma za afya ili kuboresha utoaji wa huduma,” alisema Dk Ilomo.
Aliongeza kuwa mchango huo kutoka Apotheker unakwenda sambamba na juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya afya ya kidijitali.
“Apotheker wamechukua hatua ya kuigwa kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha uwezo wa kidijitali wa kituo hiki,” alibainisha Dk Ilomo.
Alisisitiza kuwa kwa vifaa vipya vya ofisi na TEHAMA, wataalamu wa afya dijitali katika kituo hicho watakuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi, jambo litakaloongeza tija na ubunifu wao.
SOMA: Serikali kuboresha mazingira watafiti Tehama
Aidha, Dk Ilomo pia alitoa wito kwa wadau wengine kuisaidia CDH ili kuhakikisha ukuaji na mchango wake unaendelea katika sekta hiyo nyeti.
“Tunakaribisha wadau wote wanaotaka kushirikiana nasi, mradi wazingatie maadili na kanuni za utumishi wa umma,” alisisitiza.
Alikumbusha kuwa afya dijitali si hiari tena bali ni eneo la lazima la uwekezaji katika sekta ya afya.
“Tunahitaji kujitolea kuwekeza kwenye mifumo ya afya dijitali ili kupata matokeo ya maana. Mazingira wezeshi kama haya ndiyo msingi wa mafanikio katika sekta hii,” aliongeza.
Dkt. Ilomo alikiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali, hasa zile za muingiliano kati ya mifumo ya kidijitali (interoperability), na kusema kuwa kuwepo kwa timu iliyojiandaa kutasaidia kuzitatua.
Kwa upande wake, Dk Angel Dilip, Mkurugenzi wa Mradi wa Apotheker, alisema taasisi hiyo inajivunia kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa njia ya kidijitali.
“Tupo hapa kwa niaba ya timu ya Afya Tech, inayotekeleza miradi ya afya dijitali inayoongozwa na Apotheker kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na CDH,” alisema.
Dk Dilip alieleza kuwa mradi wa Afya Tech unalenga kuwaunganisha watoa huduma muhimu wa afya katika ngazi ya jamii, wakiwemo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, maduka ya dawa na vituo vya afya.
“Tumeweka mfumo wa teknolojia unaowaunganisha watoa huduma hawa watatu, ili mwananchi aweze kupata huduma kutoka popote kati ya maeneo hayo matatu bila usumbufu,” aliongeza.
Alisisitiza kuwa Apotheker itaendelea kushirikiana na serikali, si tu kupitia mradi wa Afya Tech bali pia kwenye miradi mingine ya afya dijitali inayolenga kuboresha huduma za afya.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya iliunda Kituo cha Afya Dijitali (CDH) jijini Dodoma ili kuratibu na kuimarisha matumizi ya suluhisho za kidijitali katika sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya afya ya kidijitali nchini.
Apotheker Health Access Initiative (AHAI) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa nchini mnamo Aprili 2021 na kusajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika yasioyo ya Kiserikali ya mwaka 2002, kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa jamii kupitia utafiti, mafunzo na huduma za ushauri elekezi.
AHAI inatumia uzoefu na utaalamu wa Apotheker Consultancy kuimarisha mifumo ya afya na dawa nchini Tanzania, Afrika na hata Asia.