Aiomba TCRA kutoa elimu matumizi mitandao ya kijamii

MWANAHARAKATI na Mzalendo wa Kijamii na Kisiasa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Laurence Jumanne,ameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuunda vikundi vya kijamii kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hususan kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari ,mkoani Dar es Salaam leo Julai 5,2025 katika Uzinduzi maalum wa Kampeni ya ‘No Retreat No Surrender ‘ikiwa ni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Jumanne alieleza wasiwasi wake juu ya ongezeko la matumizi mabaya ya mitandao yanayolenga kueneza upotoshaji na chuki.

“Kwa muda sasa, tumeshuhudia watu na vikundi kutoka ndani na nje ya nchi wakijiunga kupitia mitandao ya kijamii kwa nia ya kueneza propaganda, kuchochea machafuko na hatimaye kuisukuma nchi kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa manufaa yao binafsi,” amesema Jumanne.

Ameongeza kuwa baadhi ya kampeni zinazoanzishwa mitandaoni zimekuwa na malengo ya kuhujumu amani ya taifa kwa kupotosha umma kupitia ajenda zenye misingi ya chuki na uchochezi, na kwamba zimesababisha hata mashambulizi ya maneno dhidi ya wale wanaozikosoa.

“Kikundi hiki kinataka kila mtu afuate matakwa yao, ikiwemo kuchapisha na kusambaza ajenda ambazo kwa undani wake zina nia ovu ya kufanya uhaini na kuingiza taifa katika machafuko,” ameeleza

Kwa mujibu wa Jumanne, baadhi ya Watanzania hasa vijana wamekuwa wakifuata mkumbo wa harakati hizo bila kuelewa madhara yake, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa.

“Inasikitisha kuona vijana wetu wanashiriki matusi na dhihaka dhidi ya viongozi wa juu wa serikali, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi. Sisi kama wanaharakati wazalendo na machifu hatuwezi kukubali kuona viongozi wetu wakivuliwa heshima kwa kutukanwa na kudhalilishwa,” anasisitiza

Jumanne anasisitiza kuwa ni wakati wa TCRA kushirikiana na wadau wa kijamii katika kutoa elimu ya uraia, upendo kwa taifa, na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu bila madhara ya kisiasa yanayotokana na uchochezi wa mtandaoni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button