WATU watano wamekufa na 15 wamejeruhiwa baada ya basi la Tanzanite kuacha njia na kupinduka katika mlima Saranda wilayani Manyoni mkoani Singida kwenye Barabara Kuu ya Manyoni – Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 9:30 alasiri, ikihusisha basi hilo lenye namba za usajili T916 DNU aina ya ‘Higer’ likisafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Abdul Kingwande.
Kamanda Mutabihirwa alisema basi lilipofika kwenye mteremko wa mlima huo uliopo Kijiji cha Mbwasa, dereva alishindwa kulimudu likaacha njia na kupinduka upande wa kulia wa barabara na kuua abiria wanne papo hapo. “Aidha, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo,” alisema kamanda.
Alibainisha kuwa polisi wanamtafuta dereva wa basi hilo kwa kuwa alitoroka baada ya ajali. Kamanda Mutabihirwa aliwataja waliokufa ni Diwani wa Kata ya Kinampanda Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Winjuka Mkumbo (40) na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Alicia Fulgence.
Marehemu wengine watatu hawakutambuliwa na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Alisema majeruhi watano walikuwa wanaendelea kutibiwa hospitalini hapo, mmoja akihamishiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa pia jijini Dodoma kwa matibabu zaidi na waliobaki waliruhusiwa.
Aliwataja majeruhi wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuwa ni Sharifati Mwipi, Rudia Kadila, Saidi Mbwana na Abdul Ramadhan.
Majeruhi mwingine, Mwamba Sita anapatiwa matibabu Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Wiki iliyopita, watu sita walikufa kwenye ajali ya gari ndogo lililokuwa likisafiri kutoka Arusha kwenda Mwanza. Gari hilo liliacha njia likapinduka katika Kijiji cha Iguguno Shamba wilayani Mkalama. Pia Jumanne wiki hii watu 19 walifariki dunia baada ya lori lililokuwa na kontena lenye mchanga kugonga magari matatu mkoani Mbeya. Ajali hizo zimetokea siku chache tangu kutokea ajali katika mikoa ya Tanga, Shinyanga na Mtwara na kupoteza maisha ya watu zaidi ya 50. Ajali zote hizo zimetajwa chanzo kuwa ni uzembe wa madereva