WATU tisa akiwemo mjamzito wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka na kutumbukia bondeni katika Mlima wa Nkondwe, wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame amesema ajali hiyo ilitokea Alasiri ya Machi 6, 2023.
Ameeleza kuwa baada ya kufika katika mlima huo gari liliserereka na kudondokea kwenye bonde kubwa lenye kina cha mita zisizopungua 75.
Amesema chanzo cha ajali hakijajulikana na Jeshi la Polisi mkoani humo wanaendelea na uchunguzi huku utambuzi wa miili ukiendelea.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dk. Alex Mrema amethibitisha vifo hivyo na kueleza kuwa kati ya waliofariki wanaume ni wawili, watoto 3, wanawake wanne akiwemo mjamzito.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akiwa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu, alitoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao.
“Kuna baadhi walikuja wakiwa na hali si nzuri, lakini mara baada ya kupata huduma za afya hapa hospitali ya Wilaya ya Tanganyika tayari hali zao zimeendelea kuimarika, tuendelee kuwaombea waliopata majeraha waweze kupona haraka,” amesema.
Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo Philbert Focus, mkazi wa Mpanda amesema wakati wamefika katika mlima huo, ghafla kwenye kona gari lilienda kwa kasi kubwa kama limekatika breki ndipo lilipomshinda dereva na kupitiliza hadi bondeni.
Naye Hamadi Kambi shuhuda wa ajali hiyo, amesema ajali ilikuwa mbaya na kwamba alishirikiana na polisi kuokoa majeruhi na kwamba watu wanne walifia mikononi mwake.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Luhafwe, Raphael Lutonja amesema eneo hilo ni baya sana na mara kadhaa kumekuwa kukitokea ajali na kusababisha vifo, huku akidai ajali hiyo akieleza ni mbaya zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amewashukuru wananchi kwa kusaidiana na serikali katika uokoaji, ikiwemo kujitolea vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwakimbiza majeruhi hospitali.