Ajali ya meli yaitikisa Korea Kaskazini

PYONGYANG: SERIKALI ya Korea Kaskazini imeanzisha uchunguzi maalum kufuatia ajali iliyotokea wakati wa uzinduzi wa meli mpya ya kivita yenye uzito wa tani 5,000, iliyozinduliwa wiki hii katika hafla rasmi iliyoandaliwa kwa heshima kubwa.

Taarifa kutoka Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) zinasema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya sehemu ya chini ya meli hiyo kuvunjika ghafla, hali iliyozua taharuki kubwa miongoni mwa viongozi na wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo wa kijeshi.

Ajali hiyo inaripotiwa kumghadhabisha vikali Kiongozi wa Taifa hilo, Kim Jong Un, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo. Chanzo cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa rasmi.

Kwa mujibu wa KCNA, ukaguzi wa ndani ya meli na wa kina chini ya maji uliofanywa na wataalamu wa kijeshi umebaini kuwa hakukuwa na matundu yoyote yaliyochimbika chini ya meli hiyo, kinyume na ripoti za awali zilizodai uwepo wa dosari ya miundo.

“Tume ya kiufundi imebaini kuwa muundo wa ndani haukuwa na matatizo ya wazi ya kiufundi, na chanzo halisi cha ajali kinaendelea kuchunguzwa,” ilisema KCNA.

Hadi sasa, serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu iwapo kuna majeruhi au uharibifu mkubwa uliotokea kufuatia tukio hilo.Pia haijawekwa wazi iwapo meli hiyo itazinduliwa tena baada ya marekebisho kufanyika.

Tukio hilo limezua maswali kuhusu usalama na ubora wa teknolojia ya kijeshi ya Korea Kaskazini, hasa wakati ambapo taifa hilo limekuwa likijitangaza kuwa na uwezo mkubwa wa kiulinzi katika eneo la Rasi ya Korea.

SOMA: Korea Kaskazini yapeleka wanajeshi Urusi

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button