Ajira, mishahara changamoto kwa wanahabari –Kabudi

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa ajira na mishahara kwa waandishi wa habari bado ni changamoto kubwa kutokana na idadi kubwa ya waandishi kukosa mikataba rasmi ya ajira, huku wengine wakilipwa mishahara duni.
Akizungumza leo Machi 3, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Prof. Kabudi ameeleza kuwa hali hiyo inakwamisha maendeleo ya taaluma ya uandishi wa habari na kuathiri ustawi wa waandishi wenyewe.
“Mikataba mingi haiwalindi waandishi wa habari dhidi ya hatari wanazokabiliana nazo kazini, kama vile vitisho, kushambuliwa, au kufunguliwa mashtaka kwa sababu ya taarifa wanazoandika,” amesema Prof Kabudi.
Ameongeza kuwa waandishi wengi wanaajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi, huku wengine wakifanya kazi bila mikataba yoyote rasmi. Hali hii inawaweka katika hatari ya kupoteza ajira zao bila fidia, jambo linalosababisha wasiwasi na kukosekana kwa uhakika wa kipato.
SOMA ZAIDI: Maazimio 30 Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
Aidha, amebainisha kuwa kutokuwa na ajira za kudumu kunawaathiri waandishi kwa kuwanyima fursa ya kupanga maisha yao kwa utulivu: “Mbali na masuala ya malipo, waandishi wengi hawapati bima za afya wala mafao ya kijamii kama pensheni au bima ya ajali. Kutokana na kazi zao zinazowahitaji kuhama mara kwa mara na wakati mwingine kuandika habari zenye athari kwa usalama wao, wanapaswa kuwa na ulinzi wa kutosha”.
Ili kuboresha hali ya mikataba ya waandishi wa habari, Prof. Kabudi amesema zinahitajika juhudi za pamoja kati ya serikali, waajiri, na vyama vya waandishi wa habari. Pia ameahidi kuwa wizara yake, kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na mamlaka husika, itahakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa ili kuweka mikataba rasmi yenye malipo bora na inayowalinda waandishi dhidi ya changamoto wanazokabiliana nazo kazini.



