Maazimio 30 Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

MAAZIMIO 30 yamefikiwa kati ya serikali na wadau wa vyombo vya habari, katika kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo Uhuru wa Kujieleza kama Kichocheo cha Haki Nyingine za Binadamu’ Kitaifa yanafanyika Visiwani Zanzibar leo Mei 3, 2023.

Akiwasilisha maazimio hayo kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Joyce Shebe ametaja azimio la kwanza ni mashirika na wadau wa habari kuwakutanisha pamoja waandishi na wabunge wanawake, pamoja na wanafunzi wa kike ili waweze kujadili changamoto za ukatili wa kimtandao na kuwajengea uwezo, ili waweze kutumia mitandao kwa ajili ya utetezi.

Advertisement

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ione namna ya kuharakisha mchakato wa Marekebisho ya Sheria ya Habari, ili kuwawezesha wanataaluma wa habari wa Tanzania Visiwani kupata Sheria hiyo.

“Tunaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kushirikisha waandishi wa habari katika mchakato huu wa mabadiliko ya sheria, ili kuweza kutoa mazingira mazuri kwa waandishi, ikiwemo ulinzi wa waandishi dhidi ya vitisho na vifaa vyao, ” amesema Shebe.

Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia namna ya ufuatiliaji wa kina wa vyombo vya habari vilivyosajiliwa, ili kuhakikisha vinalipa kwa wakati mishahara na stahiki nyingine za waandishi wa habari.

Maazimio mengine ni kutathmini mahitaji ya kuzipitia na kuzirekebisha sheria za habari mara kwa mara, ili ziweze kuendana na mabadiliko ya kidigiti na akili bandia (Artificial Intelligence), yanayotokea ulimwenguni hivi sasa.

Pia serikali iangalie utaratibu stahiki wa kulipa madeni yake ya matangazo kwenye vyombo vya habari kwa wakati, kama mojawapo ya jitihada ya kuvikwamua kiuchumi.

“Serikali ione umuhimu wa kuharakisha mchakato wa marekebisho ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ili iendane na muktadha na mazingira ya sasa,” amesema.

Maazimio  mengine yaliyofikiwa na wadau wa Habari ni kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza jitihada za ufuatiliaji wa maudhui kwenye mitandao ya kijamii, hususan inayodhalilisha utu na heshima na kuhamasisha vitendo visivyo vya kimaadili katika jamii.

“Mamlaka kuchukua hatua mahususi ya kudhibiti na kukomesha maudhui hayo yasiyofaa kupitia utoaji elimu, adhabu mbalimbali na kuondoa maudhui hayo,” amesema.

Aidha maazimio mengine ni kufanya upembuzi wa miradi ya mafunzo kwa waandishi na kuainisha mapungufu, ili waweze kutumia rasilimali kwa usawa.

“Kuendesha au kufadhili mafunzo ya kidigiti, mabadiliko ya tabia nchi, uchafuzi wa mazingira kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala hayo na hatimaye kuweza kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa habari, wahariri, wazalishaji na mameneja wakuu, ili kuongeza mnyororo wa thamani katika utoaji wa maudhui sahihi, masoko, na biashara kwa ustawi wa vyombo vya habari.

“Kuandaa na kuendesha midahalo wa kirika kati ya waandishi wa habari wakongwe na waandishi chipukizi kwa lengo la kuwajengea uwezo kitaaluma na kujiamini,  kuwekeza kwenye tafiti za watumiaji wa vyombo vya habari na kutumia matokeo ya tafiti hizo katika utoaji wa taarifa zenye ushahidi na kuaminika kwa jamii.

“Pia kuwekeza kwenye teknolojia ya kidijiti, ubunifu na kutumia mifumo mbalimbali ya kibiashara, ili kuongeza mapato kupitia kuzalisha maudhui yenye ubora na yanayolenga mahitaji ya watumiaji.

“Kuanzisha madawati maalumu ya kuhakiki na kuthibitisha ukweli wa habari au taarifa zinazosambazwa kwa njia ya kidigiti, ili kuzuia uzalishaji na usambazaji wa taarifa za chuki, uzushi, na upotoshaji.

“Hatua hii inalenga kujenga na kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya habari katika zama hizi za mfumuko wa taarifa.

“Kuwa mstari wa mbele kufuatilia na kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujieletea maendeleo endelevu, “amesema.

Maazimio mengine ni kutengeneza na kuimarisha utekelezaji wa sera za masuala ya kijinsia kwenye vyombo vya habari na kuanzisha madawati ya jinsia, ili kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari.

“Kuripoti taarifa za maeneo ya pembezoni na kupaza sauti za wasio na sauti, ili kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi; waandishi wa habari kutumia nafasi zao kupaza sauti za wanawake na makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu na wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi.

“Pia,  kujenga mazoea na utamaduni wa kujisomea pamoja na kuwa wabunifu kupitia kujifunza stadi mpya za kidijiti ili kuendana na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika tasnia na sekta nzima ya habari duniani; waandishi wa habari wanawake kutumia fursa za kidijitali kujiendeleza kiujuzi na kiuchumi, kutangaza kazi zao, na mafanikio huku wakizingatia usalama wao watumiapo mitandao ya kijamii.

“Waandishi wa habari kujiunga katika mashirika na taasisi za habari zilizosajiliwa ili kupata usaidizi wakati wanapopatwa na kadhia mbalimbali, pamoja na kupata fursa za kihabari zinazotolewa mfano mafunzo mbalimbali,” amesema.

Maazimio mengine ni kwa taasisi za mafunzo ya uandishi wa habari kujumuisha masuala ya ulinzi na usalama wa waandishi na kozi ya matumizi ya kidigiti katika mitaala ya mafunzo kwa waandishi wa habari.

Amesema lengo ni kuwawezesha wanafunzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya kidigiti pamoja na kitisho cha usalama wa wanahabari.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *