MKURUGENZI wa Kampuni ya Rock Solution, Zacharia Nzuki amesema atawakatia bima ya afya watoto 150 wanaoishi katika mazingira magumu.
Watoto watakaonufaika na Bima hizo za afya ni kutoka vituo vya Kahama Peace Orphanage Center, New Hope pamoja na Mvuma Family vilivyopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa chakula cha pamoja na watoto hao katika sherehe ya Krismasi, Mkurugenzi huyo alisema ameguswa na mazingira magumu wanayoishi watoto hao, hasa wanapopatwa na changamoto za kiafya, ndio maana ameamua kuwakatia bima za afya, kwani hata yeye ametokea katika mazingira kama hayo.
Kampuni hiyo inayojihusisha na usambazaji wa vifaa vya migodini, pia imekuwa na utaratibu wa kusomesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kisha kuwapatia ajira pindi wanapohitimu masomo yao.
” Kampuni yetu ni kubwa tunaamini kwamba tunachokipata sio chetu kuna watu ambao wanahitaji kusaidiwa, kwa hali ya kawaida sisi tungekuwa tumeita marafiki zetu tunafurahi nao, lakini leo tupo hali ya chini kabsa kuweza kusherekea na watoto wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema Nzuki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Kahama Peace Orphanage, Halima Hamza amewaomba wadau wengine kujitokeza, ili kumsaidia baadhi ya mahitaji kituoni kwake.